Saturday, September 3, 2016

SHAURI LA KESSY DHIDI YA SIMBA LAPIGWA KALENDA

KAMATI ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji imeahirisha kikao chake kilichokuwa kikae leo kutoa hukumu ya shauri la mchezaji Hassan Ramadhan Kessy.
Simba inadai Kessy kavunja mkataba kwa kuanza kufanya mazoezi na Yanga sambamba na kusajili katika timu hiyo ya Mtaa wa Jangwani, Dar es Salaam kabla ya mkataba wake kufika mwisho Juni 15, 2016.
Akizungumza na wandishi wa habari jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, Alfred Lucas, alisema kwa mujibu wa taarifa ya kamati hiyo, shauri hilo lilisikilizwa baadaye mwezi huu katika tarehe itakayopangwa hapo baadaye kwa sababu akidi ya wajumbe wa kamati hiyo haijatimia .
"Kamati imeahirisha kikao kwa sababu akidi ni lazima wajumbe zaidi ya watatu wathibitishe kushiriki hivyo hawajatimia ndio maana kikao hicho kimeahirishwa", alisema Lucas
Shauri hilo lilikuwa lisikiliwe leo baada ya kushindikana kusikilizwa kwa shauri jingine linalohusu Klabu Simba ikiilalamikia Klabu Yanga, kuingia mkataba na mchezaji Hassan Ramadhani Kessy wakati bado ana mkataba na Simba.
Shauri la Simba dhidi ya Yanga lilishindika kusikilizwa kwa sababu Yanga hawakutokea mbele ya kamati hiyo wakati wa kusikiliza shauri hilo Agosti 24, kama hawatatokea tena, shauri hilo litasikilizwa upande mmoja na kutolewa uamuzi upande mmoja.
Kadhalika mashauri mengine yatakayosikilizwa hapo baadaye ni pamoja na yale ambayo wahusika walipewa nafasi ya kuyamaliza nje ya kamati lakini wakashindwa.