Monday, September 26, 2016

SMALLING AMSAPOTI NAHAODHA WAYNE ROONEY, ASEMA NI MTU MKUU!

Chris Smalling amemsapoti Wayne Rooney na kutamka huyo ndie 'Mtu Mkuu' kwa Manchester United na England.
Kauli hii imekuja baada ya Jumamosi Rooney kupigwa Benchi na Meneja Jose Mourinho kwenye Mechi ya EPL, Ligi Kuu England, dhidi ya Mabingwa wa England Leicester City ambayo Man United walishinda 4-1 huku Bao zao zote zikifungwa Kipindi cha Kwanza.
Kuhusu kumtema Rooney, Mourinho alitoboa uchezaji wake umeathiriwa na kupondwa mno wakati akiichezea England ambayo yeye pia ndie Kepteni kama alivyo kwa Man United.
Mara baada ya Mechi hiyo na Leicester, Mourinho alipasua kuwa Wayne Rooney bado ni Mchezaji mkubwa kwa Timu yao.

Mourinho alisema ana imani yote kwa Rooney na kuwa bado ni Mchezaji muhimu kwa Timu yao licha ya kumuanzisha Benchi.
Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Rooney kutoanza Mechi chini ya Mourinho na mara ya mwisho kwa Kepteni huyo kupigwa Benchi ni Desemba 26 Mwaka Jana.
Mourinho alieleza: "Ni Mtu wangu, namuamini kwa kila kitu. Yeye ana furaha kama mimi na hii ndiyo Timu."
Aliongeza: "Yeye ni Mchezaji mkubwa kwangu mimi, United na ni Mchezaji mkubwa kwa Nchi hii!"
Kwenye Mechi hiyo na Leicester Rooney, ambaye wakati akiwa Benchi alishangilia kila Goli la Man United kwa furaha kubwa, aliingizwa Dakika ya 83 na kuzua mjadala mkubwa huko England na Dunia yote ya Soka lakini, Smalling, ambae alivaa utepe wa Unahodha kwenye Mechi hiyo, amesema hana wasiwasi Rooney atang'ara tena.Smalling amesema: "Rooney alibaki yule yule kabla ya Gemu. Aliongea sana kama alivyo Siku zote."
"Bila kujali hali ilivyo, kwa Gemu yeyote ile bila kujali kapangwa au la, Siku zote yeye ni Mtu yule yule tu. Ndio maana yeye ndie Mtu Mkuu kwa England na Mtu Mkuu kwetu sisi!"
Smalling aliongeza: "Yeye ni Mtu mzoefu sana na amecheza Gemu nyingi sana na najua atarudia tena na kutingisha kwa sababu ana kipaji!"