Tuesday, September 13, 2016

UEFA CHAMPIONS LEAGUE: MECHI YA CITY v MONCHENGLADBACH YAKWAMISHWA NA MVUA KUBWA LEO.

Mechi ya Kwanza ya Kundi C lailiyokuwa ichezwe huko Etihad, Jijini Manchester, England kati ya Wenyeji Manchester City na Klabu ya Germany Borussia Monchengladbach imeahirishwa kutokana na Hali ya Hewa mbaya.

Mechi hiyo, moja ya Mechi 8 za UCL ambazo zilitakiwa zichezwe Leo, imeahirishwa baada ya ukaguzi wa Uwanja na Waamuzi wa Mechi hiyo wakiongozwa na Refa Bjorn Kuipers kutoka Holland kufuatia kufurika Maji kutokana Mvua kubwa iliyolikumba Jiji la Manchester.

Kwa mujibu wa Kanuni za UEFA, ikiwa Mechi itashindwa kuchezwa kwa sababu yeyote inapaswa kuchezwa Siku ya Pili au Siku itakayopangwa tena na Uongozi wa UEFA na uamuzi huo unapaswa kufanywa ndani ya Masaa Mawili baada ya kuamua kuifuta Mechi kwa kushauriana na Klabu mbili husika na Vyama vya Soka husika lakini kukiwa na mvutano kuhusu uamuzi huo, UEFA itapanga Tarehe mpya na uamuzi huo ni wa mwisho.