Thursday, September 22, 2016

WAYNE ROONEY AJIBU WANAOPONDAJI MAN UNITED, ASEMA UNITED ITAPIGANIA UBINGWA MSIMU HUU!

KEPTENI wa Manchester United Wayne Rooney Leo amewajibu Watu wanaoiponda Timu yake hasa baada ya kufungwa Mechi 3 ndani ya Siku 8 mikononi mwa Manchester City, Feyenoord na Watford.
Akiongea kwenye Kipindi cha MUTV, Kituo cha TV cha Man United, Rooney alikiri ni kawaida wao kupondwa kutokana na hadhi yao na kusema: “Hiyo ndio Soka, nadhani. Hatukushinda Gemu 3 na ni wazi kila Mtu ataongea hilo. Tulikuwa na Wiki mbaya, Siku 8 mbaya na tulipoteza Gemu 3 na muhimu ni jinsi tutakavyoibuka upya.”
Kuhusu yeye binafsi kupondwa kwa madai kiwango chake kushuka, Rooney alisema: “Ndio, nimeandamwa na hilo maisha yangu yote ya Soka na nadhani hilo ndio Soka la sasa. Mie nasikiliza Makocha wangu na Wachezaji wenzangu, Watu wa karibu yangu, na sisikilizi vitu wanavyoongea Watu wengi kwani mengi ni takataka!”

“Inabidi nitie mkazo, nifanye kazi kwa bidii, kama nilivyokuwa nikifanya maisha yangu yote ya Soka nikifanya juhudi na kujaribu kila kitu kwa faida ya Timu.”

Pia Rooney aligusia ushindi wao wa 3-1 dhidi ya Northampton kwenye Mechi ya Raundi ya 3 ya EFL CUP, Kombe la Ligi, na kusema: “Jana Usiku tulishinda na sasa tuna Gemu 3 za Nyumbani kabla ya mapumziko ya Mechi za Kimataifa na ni muhimu tushinde zote ili Msimu wetu urudi kwenye Reli.”

Kuhusu kupangwa kucheza na Mahasimu wao Man City kwenye Raundi ya 4 ya EFL CUP, Rooney ameeleza: “Kwangu mimi ni Droo safi. Baada ya kilichotokea kwenye Ligi, hii ni nafasi safi kulipa kisasi. Ni Mechi safi Old Trafford!”

Pia Rooney amesema ana hakika Man United itakuwemo kwenye mbio za Mataji Msimu huu hasa kwa vile Meneja wao ni Jose Mourinho.
Rooney ametamka: “Yeye amekuwa bora tangu aje. Mazoezi yamebadilika mno. Kila kitu kuelekea Mechi, mbinu, mwelekeo, ni mzuri sana! Nina hakika tutarudi kupigania Taji Msimu huu!”