Wednesday, October 19, 2016

FA YAMPA MOURINHO HADI IJUMAA AJIELEZE KAULI YAKE JUU YA REFA!

FA, Chama cha Soka England, kimemwandikia Meneja wa Manchester United Jose Mourinho ikimtaka ajieleze kuhusu matamshi yake juu ya Refa Anthony Taylor ambae Jana Jumatatu alichezesha pambano la Liverpool na Man United huko Anfield na kwisha 0-0.
FA imempa Mourinho hadi Ijumaa Saa 2 Usiku, Saa za Bongo, kutoa maelezo yake.
Uamuzi huo wa FA umekuja baada ya Chama hicho kuona amevunja Sheria kwa kuongea kuhusu Marefa kabla ya Mechi wanayopangiwa.
Mara baada ya Refa Taylor, mwenye Miaka 37 na anaetoka Kitongoji cha Wythenshawe kilichopo Maili 6 tu toka Old Trafford Nyumbani kwa Man United huko Jijini Manchester, kuteuliwa kuliibuka malalamiko, na hasa Mashabiki wa Liverpool, ambao walilivalia njuga kwenye Mitandao ya Kijamii..
Hata Keith Hackett, Refa wa zamani na Mkuu wa zamani wa Kampuni ya Marefa PGMOL, alisema kutaibuka malamiko makubwa ikiwa Refa huyo atafanya kosa lolote kwa upande wowote ule.
Akiongea na Wanahabari kabla ya Mechi hiyo, Mourinho aliulizwa kuhusu uteuzi wa Refa huyo na yeye kujibu: “Nadhani Bwana Taylor ni Refa mzuri sana lakini anapewa presha kubwa na itakuwa ngumu kwake kuwa na kiwango kizuri cha kuchezesha.”

Aliongeza: “Sitaki kuzungumza mengi kuhusu hili. Ninayo maoni yangu lakini nishapata fundisho kwa kuadhibiwa mara nyingi kuhusu kauli zangu kwa Marefa!”

FA sasa inataka maelezo kutoka kwa Mourinho kwa kuvunja Sheria iliyotungwa Mwaka 2009 inayokataza Mameneja kuongea lolote kuhusu Marefa kabla ya Mechi.

Meneja wa kwanza kabisa kusulubiwa kwa Sheria hiyo alikuwa ni Meneja wa zamani wa Man United, Sir Alex Ferguson, ambae alishitakiwa Mei 2011 kwa kutoa kauli kuhusu Refa Howard Webb ambayo haikuwa mbaya bali ilikuwa ya kumsifia pale aliposema alikuwa ni Refa Bora huko England.