Tuesday, October 25, 2016

JOSE MOURINHO AWAPA CHANGAMOTO WACHEZAJI MANCHESTER UNITED

Man United baada ya kulambwa 4-0 huko Stamford Bridge na Chelsea kwenye EPL, Ligi Kuu England, Juzi Jumapili, Manchester United sasa wanarudi kwao Old Trafford kujikusanya upya ili kuwavaa Mahasimu wao wakubwa Man City Jumatano kwenye Mechi ya Raundi ya 4 ya EFL CUP.
Kuelekea kwenye Dabi hii ya Jiji la Manchester, Meneja wa Manchester United, Jose Mourinho, amewataka Wachezaji wake kujibu mapigo na kuonyesha wao ni ‘Wanaume’.
Akiongea na MUTV, Kituo cha TV cha Man United, Mourinho ameeleza: “Ningependelea tucheze kwenye EPL. Tuna usongo na Ligi. Imetuweka hapa lakini pengo na Vinara ni Pointi 6.”
Amesema: “Tumekuwa na Mechi ngumu mfululizo. Tumepoteza Pointi Wikiendi hii na hata ile Mechi tulicheza na Stoke tulicheza vizuri na kupoteza Pointi kwa Droo ya 1-1. Sasa tunahitaji kushinda Mechi!”
Aliongeza: “Sisemi ni Mechi rahisi lakini sasa tuna Mechi na Burnley, tunao Swansea, West Ham, Sunderland, Middlesbrough…tunahitaji kushinda hizi!”
Mourinho alifafanua: “Timu 4 za juu, au 5 za juu, inabidi zicheze zenyewe kwa zenyewe kama sisi tulipocheza na Chelsea na Liverpool. Watapoteza Pointi, kwa hiyo bado tupo kwenye mbio za Ubingwa lakini hatuna pa kujificha!”
Alimalizia: “Tunasikitika sana sana lakini haya si ya Watoto, haya ni kwa Wanaume…lazima tuwe Wanaume na kuifanyia kazi Mechi ijayo!”