Monday, October 31, 2016

JOSE MOURINHO HATARINI KUFUNGIWA KUKANYAGA UWANJANI

BOSI wa Man United Jose Mourinho yupo hatarini kufungiwa kwa mara ya pili katika Misimu Miwili kukanyaga Uwanjani wakati Timu yake ikicheza baada ya kukwaruzana na Refa .
Juzi wakati Man United ikitoka 0-0 na Burnley katika Mechi ya EPL, Ligi Kuu England, Mourinho alitolewa kwenye Benchi na kuamriwa kukaa Jukwaa la Watazamaji Uwanjani Old Trafford baada kuzozana na Refa Mark Clattenburg baada kuwanyima Man United Penati ya wazi pale Matteo Darmian alipoangushwa na Mchezaji wa Burnley Jon Flanagan.
Kawaida Kifungo cha kutokanyaga Uwanjani huwa ni Mechi moja lakini kwa vile Msimu uliopita alipewa Adhabu kama hiyo wakati akiwa Chelsea kwa kuzozana na Refa Jon Moss Chelsea ilipofungwa na West Ham huko Upton Park, safari hii huenda akafungiwa Mechi 2 au zaidi.
Ikiwa hilo litatendeka basi Mourinho itabidi asikanyage Liberty Stadium Jumapili hii wakicheza na Swansea na pia kutotia Mguu Old Trafford Man United ikicheza na Arsenal hapo Novemba 19.
Hivi sasa FA, Chama cha Soka cha England, kinasubiri Ripoti ya Refa Clattenburg ili kuamua kama wamfungulie Mashitaka Mourinho au la.
Ikiwa atashitakiwa hii itakuwa mara ya pili kwa Mourinho Msimu huu kulikabili rungu la FA kwani hivi sasa yupo na Shitaka jingine analopaswa kulijibu Leo kabla Saa 3 Usiku kutokana na matamshi yake kuhusu Refa Anthony Taylor kabla ya Mechi yao na Liverpool mapema Mwezi huu.
Ingawa maneno ya Mourinho kuhusu Refa Taylor hayakuwa mabaya lakini yalivunja Sheria inayokataza Mameneja kuzungumzia Marefa kabla Mechi walizopangiwa.