Friday, October 14, 2016

JUMATATU PATASHIKA EPL ANFIELD, LIVERPOOL vs MAN UNITED

KLABU za Liverpool na Manchester United zimetoa tamko la pamoja kuwaonya Mashabiki kuhusu madhara ya kufanya vitendo kinyume na tabia safi za Jamii wakati wa mtanange wao wa Jumatatu Usiku Uwanjani Anfield Jijini Liverpool.
Hiyo itakuwa ni Mechi ya nadra sana kwa Timu hizo kupambana Usiku kwenye Mechi za Nchi yao ingawa Msimu uliopita walipambana Usiku kwenye Mashindano ya UEFA EUROPA LIGI na kuzua tafrani na UEFA ambayo ilizichunguza Klabu hizo na hatimaye kuziadhibu kutokana na kushangilia kwa kashfa kwa Mashabiki wao ambao pia walileta vurugu.

Klabu hizo mbili kubwa huko Uingereza zenye upinzani wa Jadi zimewania kupoza uhasama hasa ule wa kila upande kukashifu maafa yaliyozikumba Klabu hizo Miaka ya nyuma yakiwa ni yale ya Hillsborough, kwa Liverpool ambapo Mashabiki wao wengi walikufa Uwanjani kutokana na mkanyagano na ile Ajali ya Ndege ya Munich iliyoua Wachezaji wa Man United.

Katika Taarifa yao ya pamoja, Klabu hizo zimesema: “Klabu zote mbili, Mashabiki wao na Wapenzi wa Soka Dunia nzima wanangojea kwa hamu pambano hili la kihistoria na lenye hisia kubwa zenye upinzani mkubwa na wa Miaka mingi kupita yote. Upo upinzani mkubwa kati ya Mashabiki wetu na tunawaomba Mashabiki wote wawe na heshima na wasaidie kufuta namna zote za tabia za kuudhi na kubaguana kwenye Gemu hii.”
Taarifa hiyo ikaonya: “Shabiki yeyote akikutwa anashiriki vitendo vyovyote viovu na Walinzi au kunaswa kwenye Kamera za Ulinzi ataondolewa mara moja toka Uwanjani na kuwa hatarini kukamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi na kushitakiwa pamoja na kuwekewa taarifa za kuzuiwa kabisa kuingia tena Uwanjani!”
Pambano hili la Jumatatu ni Mechi ya EPL, Ligi Kuu England.


JE WAJUA?
-Mtanange wa Liverpool dhidi ya Manchester United ni pambano kubwa Duniani linalotazamwa na Watu Milioni 700 kwenye Nchi 200.