Sunday, October 16, 2016

LIVERPOOL vs MANCHESTER UNITED KESHO JUMATATU, REFA ANTHONY TAYLOR ATAKUWA NA WAKATI MGUMU!

MENEJA wa Manchester United Jose Mourinho ameeleza kuwa Refa Anthony Taylor, ambae amepangwa kuchezesha pambano la Jumatatu Usiku huko Anfield la EPL, Ligi Kuu England, kati ya Mahasimu wakubwa Liverpool na Man United, atakuwa na wakati mgumu.
Uteuzi wa Refa huyo umepondwa na Watu kadhaa na hasa Mashabiki wa Liverpool ambao wamelivalia njuga kwenye Mitandao ya Kijamii.

Akimwelezea kuwa Refa huyo ni mzuri, Mourinho pia amedai Watu kwa makusudi wanamletea Refa huyo presha.
Professional Game Match Officials Limited (PGMOL), Mamlaka inayosimamia Marefa wa Gemu za Kulipwa, ndio huteu Marefa na imemteua Anthony Taylor, mwenye Miaka 37 na anaetoka Kitongoji cha Wythenshawe kilichopo Maili 6 tu toka Old Trafford Nyumbani kwa Man United huko Jijini Manchester, kuwa Refa wa Mechi hiyo.
------------------------------------------
JE WAJUA?
-Uso kwa Uso:
-Liverpool Ushindi 75 Sare 62 Man United Ushindi 87

-------------------------------------------
Keith Hackett, Refa wa zamani na Mkuu wa zamani wa PGMOL, amezungumzia uteuzi wa Refa Anthony Taylor na kusema kutaibuka malamiko makubwa ikiwa Refa huyo atafanya kosa lolote kwa upande wowote ule.

Mwezi Aprili Mwaka huu, Refa Kevin Friend aliondolewa kuchezesha Mechi ya Tottenham Hotspur na Stoke City baada ya kuibuka dhana ya Refa huyo kuisapoti Leicester City ambayo wakati huo ilikuwa ikichuana vikali na Tottenham kutwaa Ubingwa wa England ambao hatimaye ulitwaliwa na Leicester City.
Mwaka 2014, Meneja wa Liverpool wakati huo, Brendan Rodgers, alipigwa Faini na FA, Chama cha Soka England, baada ya kulaumu uteuzi wa Refa Lee Mason kusimamia Mechi na Manchester City huko Etihad Stadium ambayo walifungwa 2-1.
Brendan Rodgers alidai: “Nilishangaa tunacheza Jijini Manchester na Refa anatoka Jijini Manchester! Natumaini Siku zijazo hatutakuwa na Refa wa Jijini Manchester kuchezesha Mechi ya Liverpool dhidi ya Manchester United!”
Hata hivyo, baadhi ya Wachambuzi wakubwa wa Soka huko England wameppuza madai.kuhusu Refa Anthony Taylor na kutaka Watu kutilia mkazo Gemu yenyewe na si ushabiki usiokuwa na msingi.