Wednesday, October 19, 2016

TOKA TFF: KICHUYA BORA, LIGI DARAJA LA 2 KUANZA OKT 29, VPL TIMU 12 DIMBANI LEO!

KICHUNYA MCHEZAJI BORA SEPTEMBA VPL
Mshambuliaji Shiza Kichuya wa Simba SC amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa Septemba msimu wa 2016/2017.
Kichuya ambaye ni mshambulaji aliwashinda wachezaji Adam Kingwande wa Stand United na Omari Mponda wa Ndanda FC.
Mchezaji aliisadia timu yake kwa mwezi huo kupata pointi zote 12 katika mechi nne ilizocheza, matokeo ambayo yameifanya Simba iendelee kuongoza Ligi hiyo inayoshirikisha timu 16. Pia alifunga mabao matatu katika mechi mbili kati ya nne ilizocheza timu yake.
Kwa kushinda tuzo hizo ya mwezi, Kichuya atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom Tanzania.

LIGI DARAJA LA PILI KUANZA OKTOBA 29, 2016
Timu 24, zinatarajiwa kupambana katika michuano ya Ligi Daraja la Pili msimu wa 2016/17 kuanzia Oktoba 29, mwaka huu, imefahamika.

Timu hizo zimepangwa katika makundi manne yenye timu sita kwa kuangalia zaidi jiografia au kanda ambako timu imetoka – lengo likiwa kupunguza gharama kwa timu shiriki hasa ikizingatiwa kuwa michuano hiyo haijapata mdhamini hadi sasa.
Kundi A lina timu za Mashujaa ya Kigoma, Mirambo ya Tabora, Mji Mkuu ya Dodoma, Green Warriors ya Pwani, Bulyanhulu na Transit Camp za Shinyanga.
Mechi za kwanza zitakuwa ni kati ya Mashujaa dhidi ya Green kwenye Uwanja wa Tanganyika mjini Kigoma wakati Mirambo itaikaribisha Mji Mkuu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi. Timu za Transit Camp na Bulyanhulu zitacheza Oktoba 30, mwaka huu.
Kundi B; African Wanderers ya Iringa itaikaribisha AFC ya Arusha kwenye Uwanja wa Kichangani mjini Iringa siku ya Oktoba 29, 2016 wakati Kitayosa itakuwa mgeni wa Madini kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Timu nyingine kwenye kundi hilo ni Pepsi ambayo itacheza na JKT Oljoro Oktoba 30, mwaka huu.
Kundi C; Villa Squad itafungua dimba na Kariakoo ya Lindi kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam wakati Burkinafaso ya itaikaribisha Abajalo kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Timu nyingine kwenye kundi hilo ni Cchanganyikeni na Cosmopolitan za Dar es Salaam.

Kundi D; Namungo ya Lindi itafungua dimba na Sabasaba kwenye Uwanja wa Sokoine ulioko Nachingwea mkoani Lindi wakati Mkamba Rangers itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Mkamba kuikaribisha Mawenzi Market kwenye Uwanja wa Mkamba ulioko Morogoro.

VPL: TIMU 12 UWANJANI KESHO, AZAM NA MTIBWA SAA 1.00 USIKU
Wakati leo Jumanne Oktoba 18, 2016 timu ya JKT Ruvu ya Pwani na Kagera Sugar zinafungua rasmi mzunguko wa 11 wa Ligi Kuu ya Mpira wa Miguu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), michezo mingine sita itafanyika kesho Jumatano Oktoba 19, mwaka huu wakati keshokutwa Alhamisi Oktoba 20, kutakuwa na mchezo mmoja tu.
Mchezo wa leo Na. 86 wa VPL utafanyika Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani kabla ya kesho Oktoba 19, mwaka huu kuendelea kwa mechi sita pia za mzunguko 11 wa kukamilisha raundi ya kwanza kwa msimu 2016/17.
Vodacom – Kampuni ya simu za mkononi inayoongoza nchini kwa kutoa huduma za kisasa za mawasiliano ndiyo mdhamini mkuu ligi hiyo ikisaidiana kwa karibu sana Kampuni ya kisasa ya vyombo vya habari yenye kurusha vipindi vyake kwa weledi na ubora wa hali ya juu ya Azam Televisheni (Azam Tv) na DTB- Benki ya kuaminika nchini kwa usalama wa fedha zako.

Kampuni hizo zinazong’arisha VPL, kesho zitakuwa sambamba kwenye kuchagiza michezo ya Ruvu Shooting ya Pwani ambayo itaikaribisha Mwadui ya Shinyanga kwenye Uwanja wa Mabatini uliuoko Mlandizi mkoani Pwani katika mchezo Na. 81 wa VPL utakaoanza saa 10.00 jioni.

Mchezo Na. 82 utakaozikutanisha Azam FC ya Dar es Salaam na Mtibwa Sugar ya Morogoro utafanyika saa 1.00 usiku (19h00). Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Azam ulioko Chamazi – maskani ya Azam yalioko nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam wakati mchezo Na. 83 utazikutanisha timu za Ndanda FC na Mbeya City ya Mbeya kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Mchezo Na. 85 utazikutanisha timu za Tanzania Prisons ya Mbeya na Stand United itakayokuwa mgeni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya huku mechi Na. 87 itazikutanisha Toto African ya Mwanza itakayocheza na Young Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati African Lyon itakuwa mwenyeji wa Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam kwenye mchezo Na. 88.

Ligi hiyo itaendelea tena keshokutwa Alhamisi Oktoba 20, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ambako vinara wa ligi hiyo kwenye msimamo hadi sasa, Simba itakuwa mwenyeji wa Mbao FC ya Mwanza katika mchezo Na. 84.