Sunday, October 16, 2016

VPL: YANGA DHIDI YA AZAM PUNDE LEO!

BAADA ya Simba Jana kuzitimulia vumbi Timu nyingine za VPL, Ligi Kuu Vodacom, kwa kuichapa 2-0 Kagera Sugar na kuzidi kutokomea kileleni, Leo tena Uwanja wa Uhuru utatumika kwa Mechi kali kati ya Mabingwa Watetezi Yanga na Azam FC.
Hii ni Mechi muhimu mno kwa Timu hizo 2 kwani kufungwa kutazitupa mbali na Vinara Simba.
Hivi sasa Simba wana Pointi 23 kwa Mechi 9 wakati Yanga ni wa 3 wakiwa na Pointi 14 kwa Mechi 7 na Azam wako Nafasi ya 9 wakiwa na Pointi 11 kwa Mechi 8.
Azam FC, chini ya Kocha toka Spain Zeben Hernandez, wanaingia kwenye Mechi hii ya Leo wakiwa kwenye wimbi la Mechi 4 bila ushindi lililoanzia kwa vipigo toka kwa Simba na Ndanda FC, Sare na Ruvu Shooting na kisha kufungwa na Stand United.
Yanga, chini ya Kocha Mholanzi Hans van Pluijm, Juzi waliibandika Timu ngumu Mtibwa Sugar 3-1.
Lakini, kwenye VPL, Timu hizi zikikutana huwezi kutabiri na Rekodi ya hivi karibuni inaonyesha wametoka Sare mara 4 na kila Timu kushinda mara 2.
Mechi nyingine ya VPL hii Leo ni kati ya Ruvu Shooting na Mbeya City.