Friday, October 14, 2016

WAPYA: STEVE BRUCE ATUA ASTON VILLA, STEVE McCLAREN NAE ADONDOKA DERBY!

WALIOWAHI kuwepo Manchester United, Steve Bruce na Steve McClaren, wamepata Klabu Mpya kama Mameneja Wapya.
Klabu ya Aston Villa, ambayo iliporomoka Daraja toka EPL, Ligi Kuu England, Mei Mwaka huu na sasa ipo Championship, imemteua Steve Bruce kama Meneja wao.
Bruce, mwenye Miaka 55 na aliewahi kuwa Kepteni wa Man United, ashawahi kuzipandisha Daraja Timu mara 4 kutinga EPL akiwa na Birmingham, mara 2, na Hull City, mara 2.
Bruce, alieamua kuachana na Hull City Mwezi Julai, anakuwa mrithi wa Roberto di Matteo aliefukuzwa Oktoba 3 na atakuwa Meneja wa 6 kwa Klabu hiyo katika Miezi 12 iliyopita.
Mechi ya kwanza kwa Bruce ni Jumamosi wakiivaa Wolves kwenye Ligi ambayo wapo nafasi ya 19.

Nae Bosi wa zamani wa England na aliewahi kuwa Meneja Msaidizi huko Man United chini ya Sir Alex Ferguson, Steve McClaren, amethibitishwa kuwa ni Meneja Mpya wa Derby County ambako aliondoka Miezi 17 iliyopita baada ya kufukuzwa.
McClaren, mwenye Miaka 55, anamrithi Nigel Pearson alieondoka Jumamosi iliyopita.
McClaren aliondoka Derby Mei 2015 huku kukiwa na msuguano baada ya kuhusishwa na kuhamia Newcastle ambako alihamia kweli na ambako alitimuliwa Machi 2016.
Hivi sasa Derby ipo Nafasi ya 20 kwenye Ligi ya Championship.