Wednesday, November 2, 2016

AZAM YAIFUMUA TOTO AFRICANS LEO BAO 1-0 VPL NA KUPANDA JUU NAFASI YA TATU!

AZAM FC kama masihara imepanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na kufikisha pointi 22 sawa na Stand United ambayo leo imechapwa na vinara Simba bao 1-0.
Azam walifanya juhudi kubwa kutafuta bao hilo kwa kulishambulia kama nyuki lango la Toto lakini hadi timu hizo zikienda mapumziko hakuna timu ambayo ilikuwa imeziona nyavu.

Kinda Shabani Iddi aliyetokea benchi ndiye alipeleka furaha Azam dakika ya 76 baada ya kumalizia kazi nzuri ya nahodha John Bocco ambaye alikuwa akihaha Uwanja mzima kuhakikisha timu inaibuka na ushindi.

Azam sasa wameanza kurudi kwenye ubora wao ambapo wamezidiwa pointi tano na wanaokamata nafasi ya pili hali ambayo imeanza kurudisha morali kwa wachezaji ambao wanaonekana kupambana kutafuta matokeo tofauti na ilivyokuwa katika mechi kadhaa zilizopita.

Mechi iliyopita Azam iliibuka na ushindi ugenini dhidi ya Kagera Sugar hali inayoonyesha kuwa wameanza kuwamulikia taa ya kijani timu za Simba wanaoizidi Yanga pointi nane huku wao Azam wakiwa nyuma ya Simba kwa pointi 13.