Wednesday, November 23, 2016

JOSE MOURINHO: IBRAHIMOVIC KUONGEZEWA MKATABA


Zlatan Ibrahimovic huenda akaongezewa Mkataba wa Mwaka Mmoja zaidi huko Manchester United.
Meneja wa Vigogo hao wa England Jose Mourinho ametoboa kuwa Man United itatumia kipengele cha uwezo wao kumwongeze Mchezaji huyo wa Sweden Mwaka mwingine mmoja baada ya Mkataba wake kumalizika mwishoni mwa Msimu huu Mwezi Juni Mwakani.
Ibrahimovic, mwenye Miaka 35, alihamia Old Trafford kama Mchezaji Huru Mwezi Julai baada ya Mkataba wake na Paris Saint-Germain ya France kumalizika na kusaini kwa Mwaka Mmoja na Man United huku kukiwa na Kipengele cha Nyongeza ya Mwaka Mmoja.
Akiongea na Wanahabari kuhusiana na Mechi yao ya Alhamisi Usiku ya Kundi A la UEFA EUROPA LIGI dhidi ya Feyenoord Uwanjani Old Trafford, Mourinho alitamka: “Mambo ni rahisi kuhusu Zlatan. Anayo 1 jumlisha 1. Tuna furaha na yeye. Tutatumia nyongeza ya Mwaka Mmoja mwishoni mwa Msimu. Baada ya hapo atafanya analotaka.”

Akiichezea Man United, Ibrahimovic amefunga Bao 8 katika Mechi 17 alizocheza.
Akigusia uwezekano wa kubakia Old Trafford kwa Msimu wa 2017/18, mwenyewe Gwiji huyo wa Sweden amesema yeye atabaki tu ikiwa ataona anastahili kubakia.
Ibrahimovic ametwaa Mataji 11 ya Ligi katika Nchi 4 na kuweka Rekodi ya Magoli kwa kuifungia Nchi yake Sweden Mabao 62 katika Mechi 116.
Hivi sasa amestaafu kuichezea Timu ya Taifa ya Sweden tangu Mwezi Juni walipotupwa nje ya EURO 2016.