Tuesday, November 15, 2016

PATASHIKA WIKIENDI HII OLD TRAFFORD JUMAMOSI MAN UNITED vs ARSENAL, REFA NI ANDRE MARRINER!

MCHEZO  kati ya Manchester United na Arsenal ambao utachezwa Jumamosi Novemba 19 huko Old Trafford Jijini Manchester ikiwa ni Mechi ya EPL, Ligi Kuu England, utachezeshwa na Refa Andre Marriner.

Hii itakuwa ni Mechi ya kwanza kwa Timu hizi kupambana Msimu huu na hii ni nafasi nyingine kwa uhasama uliozoewa wa Mameneja Jose Mourinho na Arsene Wenger kujirudia tena, uhasama ambao ulianzia huko London wakati Mourinho akiwa na Chelsea na Wenger na hii hii Arsenal yake.
Image result for MAN UNITED vs ARSENAL Andre Marriner
Refa Marriner, mwenye Miaka 45, ameshachezesha Mechi za Man United za Ligi Kuu England mara 21 Wakishinda 13, Sare 1 na Kufungwa 7 huku akitoa Kadi za Njano 33 na Kadi Nyekundu 1.

Lakini kwa Arsenal, anakumbukwa sana kwa ajili ya Gemu ya 2014 wakati Chelsea ya Mourinho ikiinyuka Arsenal ya Wenger 6-0 kwa kumpa kimakosa Kadi Nyekundu Kieran Gibbs badala ya Alex Oxlade-Chamberlain.

Bila shaka hii ndio Mechi kubwa kabisa ya EPL hadi sasa Msimu huu hasa ukitazama Man United wako Nafasi ya 6 na wanataka kupanda juu wakati Arsenal wapo Nafasi ya 4 na wao wanawania pia kukwea juu.

Baada ya Mechi 11, Liverpool ndio Vinara wakiwa na Pointi 26, Chelsea ni wa Pili wana 25, wakifuata Man City na Arsenal wenye 24 kila mmoja, Tottenham wa 5 wakiwa na 21 na Man United ni wa 6 na wana 18.

Katika Mechi zao za mwisho za EPL kabla hawajapisha Mechi za Kimataifa, Arsenal walitoka 1-1 na Tottenham katika Dabi ya London Kaskazini na Man United kuitandika Swansea 3-1 huko Liberty Stadium, Wales.