Wednesday, November 9, 2016

SIMBA HOI TENA LEO,YAKUBALI KIPIGO TENA KUTOKA KWA TANZANIA PRISONS BAO 2-1 MJINI MBEYA.

VINARA wa VPL, Ligi Kuu Vodacom, Simba Leo wameshushiwa kipigo chao cha pili mfululizo baada ya kuchapwa 2-1 na Tanzania Prisons huko Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Jumapili iliyopita, Simba, wakiwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, walifungwa 1-0 na African Lyon.

Leo, Simba walitangulia kufunga Dakika ya 43 kwa Bao la Jamal Mnyate na Prisons kusawazisha Dakika ya 47 kupitia Victor Hangaya ambae ndie pia alifunga Bao la Pili na laushindi kwa Prisons katika Dakika ya 63.
Matokeo haya yamewapaisha Tanzania Prisons hadi Nafasi ya 7 wakiwa na Pointi 19 kwa Mechi 15.

Simba wanabaki kileleni wakiwa na Pointi 35 kwa Mechi 15 lakini pengo lao na Timu ya Pili Yanga linaweza kupungua sana na kuwa Pointi 2 tu toka 8 za Wiki iliyopita ikiwa Yanga Kesho Alhamisi wataibwaga Ruvu Shooting Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Katika Mechi nyingine ya VPL iliyochezwa huko Shinyanga, Azam FC walitoka nyuma kwa Bao 1-0 la Dakika ya 30 lililofungwa na Hassan Kabunda na kuinyuka Mwadui FC Bao 4-1.

Bao za Azam FC zilifungwa Dakika za 54, 71, 74 na 77 kupitia John Bocco, Shaaban Idd, Francisco Zekumbawira na Shaaban Idd kwa mara nyingine.

Matokeo haya yameibakiza Mwadui FC Nafasi ya Pili toka mkiani wakiwa na Pointi 13 kwa Mechi 15 na Azam FC kuchupa hadi Nafasi ya 3 wakiwa na Pointi 25 kwa Mechi 15.