Saturday, November 12, 2016

TAIFA STARS WAKIJIANDAA KUPAMBANA NA WENYEJI ZIMBABWE


Taswira za mazoezi ya Taifa Stars mjini Harare kujiandaa kupambana na timu ya taifa ya Zimbabwe

Timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro kutoka Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) inatarajiwa kucheza na Zimbabwe katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika Uwanja wa Michezo wa Taifa wa Zimbabwe ulioko hapa jijini Harare.

Taifa Stars iliyotua jana jijini hapa na kufikia Hoteli ya The Rainbow Towers, inacheza mchezo huo ikiwa na shauku ya ushindi baada ya kuporomoka kiwango chake kutoka nafasi ya 132 mwezi Septemba, 2016 hadi nafasi ya 144.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba amejiandaa vema na mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika jijini Harare ambao mbali ya kurushwa na kituo cha Televisheni ya Taifa cha Zimbabwe (ZBC), pia utaunganishwa na Kituo cha Televisheni cha Azam (Azam Tv) ambayo imejikita zaidi kuonyesha michezo.

Mchezo huo umeratibiwa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambalo huwa na kalenda ya wiki ya mechi za kimataifa kwa wanachama wake – Tanzania ni miongoni mwao.

Kikosi cha Taifa Stars chini ya Kocha Mkwasa kinatarajiwa kuwa Deogratius Munishi golini Michael Aidan upande wa beki ya kulia wakati kushoto atakuwa na Mohamed Hussein wakati mabeki wa kati ni Erasto Nyoni na Vicent Andrew.

Viungo ni Himid Mao na Mohammed Ibrahim wakati mawinga ni Shiza Kichuya na Simon Msuva wakati washambuliaji ni Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.

Mchezo huu utakuwa na faida zaidi kwa Tanzania kama ikiwafunga Wazimbabwe kwa kuwa itaongeza alama za nyongeza kwa kushinda ugenini.

Matokeo ya mchezo huo, ni sehemu malumu kupima viwango vya ubora na uwezo wa timu za taifa. Kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya 144 kati ya nchi 205 wanachama wa FIFA zilizopimwa ubora. Zimbambwe yenyewe inashika nafasi ya 110.

Argentina inaongoza ikifuatiwa na Ubelgiji anakocheza Mbwana Samatta – nyota wa kimataifa wa Tanzania. Samatta anacheza klabu ya K.R.C Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji. Timu nyingine bora kimataifa ni Chile, Colombia na Ujerumani.

Katika Bara la Afrika, Ivory Coast ambayo ni ya 31 kwa ubora duniani ndiyo inayoongoza ikifuatiwa na Senegal (32), Algeria (35), Tunisia (38) na Ghana (45).