Saturday, November 12, 2016

TWIGA STARS UWANJANI NAO KESHO JUMAPILI


Baada ya kupoteza mchezo wa kwanza, timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu Wanawake ‘Twiga Stars’ kesho Jumapili Novemba 13, 2016 itaingia tena uwanjani kupambana na wenyeji wao Cameroon katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika jijini Yauonde, Cameroon.

Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Sebastian Nkoma amesema amefanyia marekebisho yaliyosababisha kupoteza mchezo wa kwanza na sasa mchezo wa Jumapili huenda akalipa kisasi cha kupoteza dhidi ya wenyeji hao wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.

Katika mchezo wa kwanza mabao ya Cameroon yalifungwa na Mshambuliaji Ngoya Ajara wa Klabu ya Sundsvalls ya Sweden ambaye pia ndiye Mchezaji Bora wa mwaka 2016 nchini Cameroon wakati lile la pili lilifungwa na Kiungo wa Klabu ya Aurillac ya Ufaransa Ngono Mani Michelle katika dakika ya 71.

Twiga Stars wamealikwa na Cameroon ambao wameamua kuipa heshima Tanzania na kuona kuwa timu hiyo ina ubora wa na kwamba inafaa kuipimana ubavu kabla ya kuanza kwa fainali hizo Novemba 19, mwaka huu.

Twiga Stars ambayo sehemu kubwa ya kikosi hicho kinaundwa na wachezaji wa timu ya taifa ya Wanawake ya Tanzania Bara yaani Kilimanjaro Queens ina rekodi nzuri ya kuwa kinara wa viwango vya ubora kwa nchi za Afrika Mashariki na kati lakini zaidi ni mabingwa wapya wa ukanda huo – ubingwa uliopatikana Septemba, mwaka huu huko Uganda.

Rekodi hizo zimesukuma Shirikisho la Mpira wa Miguu la Cameroon (FECAFOOT) – nyumbani kwa Rais wa CAF, Issa Hayatou kuikubali Twiga Stars na hivyo kuomba kucheza nayo mwishoni mwa wiki hii. Tayari Twiga Stars imeanza maandalizi ya kutosha chini ya Makocha Sebastian Nkoma na Wasaidizi wake Edna Lema na El Uterry Mohrery.

Kikosi cha Twiga Stars wamo makipa, Fatma Omari na Najiat Abbas; mabeki ni Wema Richard, Sophia Mwasikili, Anastasia Katunzi, Maimuna Hamisi, Fatuma Issa, Happiness Mwaipaja na Mary Masatu wakati viungo ni Donisia Minja, Stumai Abdallah, Amina Ally, Anna Mwaisura na Fadila Kigarawa ilhali washambuliaji ni Fatuma Swalehe, Asha Rashid na Mwanahamisi Omari.