Wednesday, November 30, 2016

USIKU HUU, JOSE MOURINHO KUIKOSA MECHI YA MAN UNITED DHIDI YA WEST HAM UNITED

MENEJA wa Manchester United Jose Mourinho Usiku wa Leo hatakuwepo Benchi la Ufundi la Timu yake ikicheza Mechi ya Robo Fainali ya Kombe la Ligi, EFL CUP, na West Ham Uwanjani Old Trafford kufuatia Kifungo cha Mechi 1 na Faini ya Pauni 16,000.
Adhabu hizo zimetokana na Kosa lake la kuipiga Teke chupa ya maji wakati wa Mechi ya Jumapili walipotoka Sare 1-1 na West Ham alipokasirishwa na Refa Jon Moss kumpa Kadi ya Njano Mchezaji wake Paul Pogba badala ya wao kupewa Frikiki.
Jana Jumanne, Mourinho alikiri Kosa lake na Leo Jopo la FA, Chama cha Soka England, kumwadhibu.
Ndani ya Miezi Miwili, hilo ni Kosa la Pili kwa Mourinho baada ya Oktoba 29 kutolewa nje na kisha Kufungiwa Mechi 1 na kupigwa Faini ya Pauni 8,000.

Kabla ya hapo, Mourinho alipigwa Faini Pauni 50,000 baada ya kutoa kauli kuhusu Refa wa Mechi yao na Liverpool, Anthony Taylor, kabla ya Mechi hiyo iliyochezwa Oktoba 17 huko Anfield.

Ingawa Wachambuzi wengi waliamini kufuatia mlolongo huo wa Makosa, Mourinho safari hii angeshushiwa Rungu kali, FA imechukulia Kosa la Mourinho kupiga Teke Chupa ya Maji ni dogo na hasa kwa vile hakuwapandishia Marefa baada ya kuamriwa kutoka Uwanjani na Refa Jon Moss.

Na kama si makosa yake ya hivi karibuni, basi Mourinho angepigwa tu Faini ndogo bila Kifungo.

Hata hivyo, licha ya kufungiwa kutokaa Benchi Mechi hii ya Leo, FA imemruhusu Mourinho kuongea na Wachezaji kabla ya Mechi, wakati wa Haftaimu na pia kuwasiliana na Benchi lake wakati wote wa Mechi yeye akiwa Jukwaani.