Monday, December 5, 2016

BAADA MAAFA: CHAPECOENSE YAPEWA UBINGWA COPA SUDAMERICANA

SHIRIKISHO la Soka Marekani ya Kusini, CONMEBOL, limekubali kuipa Ubingwa wa Copa Sudamericana Klabu ya Brazil Chapecoense ambayo iliangamia kufuatia kuanguka kwa Ndege yao iliyoishiwa Mafuta wakati ikielekea kwenye Fainali ya Kombe hilo.
CONMEBOL imethibitisha uamuzi huo na pia kusema Chapecoense kutoka Mji wa Brazil Chapeco itapewa Dau la Dola Milioni kama Zawadi ya Ubingwa huo.
Chapecoense, Klabu ndogo ya Brazil iliyoshangaza wengi kwa kupanda Ligi Kuu ya Brazil na pia kufuzu kucheza Copa Sudamericana ambalo ni la pili kwa ukubwa huko Marekani ya Kusini baada ya Copa Libertadores, iliangamia Wiki iliyopita ikielekea kwenye Mechi yao kubwa kabisa katika Historia yao kwa Ajali ya Ndege iliyoua Watu 71. Chapecoense ilikuwa ikielekea huko Mjini Medellin kucheza Mechi ya kwanza ya Fainali ya Copa Sudamericana dhidi ya Atletico Nacional ambayo mara baada ya maafa hayo ilitoa wito Chapecoense ipewe Ubingwa wa Copa Sudamericana.
CONMEBOL imetamka imeitikia wito wa Atletico Nacional.
Sasa pia CONMEBOL imewapa Atletico Nacional Tuzo ya Karne ya Uchezaji wa Haki, CONMEBOL Centenary Fair Play Award. Huko Barani Ulaya, UEFA imetangaza kuwa Wiki hii, kabla ya Mechi za Mwisho za Makundi ya UEFA CHAMPIONS LIGI na zile za UEFA EUROPA LIGI, Timu zote zitasimama na kutoa Heshima ya Kimya kwa Dakika Moja kwa Chapecoense.