Saturday, December 31, 2016

COASTAL UNION ‘WAGOSI WA KAYA’ WATANGAZA KIAMA LIGI DARAJA LA KWANZA

Uongozi wa Coastal Union kutoka mkoani Tanga inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, unawataka wapenzi wake waliopo Dar es Salaam kesho (Jumapili Januari 1, 2017) kufika uwanja wa Karume zilipo ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ili kushuhudia timu mpya na yenye uwezo wa hali ya juu.

Kwa mujibu wa Meneja wa timu Hilal Said, vijana wa sasa ni wapya nah ii ni mechi ya pili tangu mzunguko wa pili uanze. Hivyo usajili mpya umeonyesha mwanga na vijana wanapiga soka la uhakika.

“Naweza kusema sisi hatustahili kucheza na timu za ligi daraja la kwanza, hata ligi kuu hakuna timu ya kutufunga kwa sasa tumekua level nyingine kabisa. Inafika wakati hata tukifanya mechi za majaribio tunaona kama tunazionea timu tunazocheza nazo.

“Hivyo nawaomba wapenzi wa soka si lazima wawe wa Coastal Union tu bali mpenzi yeyote anayependa kuona soka la uhakika aje Karume kesho Jumapili. Tunafungua mwaka kwa kuichapa Kimondo mabao yasiyo na idadi,” alisema Hilal.

Coastal Union inayoshika nafasi ya tano katika kundi B kwa sasa ina point sita huku Kimondo FC kutoka beya ikishika mkia kwenye kundi hili.
Mchezo uliopita Coastal Union ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya Polisi Morogoro katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro huku mashabiki wa soka mkoani humo wakisifia kiwango kikubwa kilichoonyeshwa na wachezaji wa Coastal Union.

Katibu wa Coastal Union, Tahbit Abuu, aliweka wazi kuwa kwa sasa timu yoyote itakayoingia katika anga zao watarajie kichapo kwani wanataka kuhakikisha mechozote sita zilizobaki wanashinda ili kujiweka katika nafasi nzuri.

“Tunataka turudi ligi kuu, hakuna namna nyingine zaidi ya kuendeleza kichapo popote pale iwe nyumbani au ugenini, kwa sababu timu ya ushindani tunayo na uwezo tunao, hatuna sababu ya kuwa wanyonge,” alisema.


Wachezaji wa Coastal Union wameshawasili jijini Dar es Salaam tangu Ijumaa ambapo wamefichwa katika kambi maalumu kwenye moja ya fukwe za Bahari ya Hindi tayari kwa mechi ya Jumapili.


Habari hii imetolewa na msemaji wa Klabu Hafidh Kido
0713 593894