Tuesday, December 20, 2016

KIFUNGO CHA REAL KUSAJILI WACHEZAJI CHAPUNGUZWA, MWAKANI RUKSA KUSAJILI WAPYA!

KILE Kifungo cha Real Madrid walichoshushiwa na FIFA cha kutosajili Wachezaji Wapya hadi Januari 2018 sasa kimepunguzwa na CAS, Court of Arbitration for Sport, Mahakama ya Usuluhishi Michezoni, na sasa wataruhusiwa kusajili Wapya kuanzia Julai, 2017.
Awali FIFA iliwafungia Real kutosajili Wachezaji Wapya kwa Madirisha Mawili ya Uhamisho ikimaanisha yale ya Januari 2017 na Julai 2017 kwa kosa la kusajili Wachezaji wa chini ya Miaka 18 kinyume na Kanuni za FIFA,
Vile vile, CAS imeipunguza Faini waliyotozwa Real kutoka Pauni 282,000 hadi Pauni 188,000.
Adhabu hiyo ya FIFA walipewa Real na pia wenzao wa Jiji la Madrid Atletico Madrid Mwezi Januari lakini Klabu hizo zilikata Rufaa na hivyo kupata mwanya wa Kusajili mwanzoni mwa Msimu Mwezi Julai.
Hata hivyo, FIFA ikazitupa Rufaa za Klabu hizo mbili na zote zikaamua kukata Rufaa kwa CAS.
Kupunguziwa Adhabu kwa Real kumetobolewa kupitia Tovuti ya Klabu hiyo lakini hamna habari yeyote kuhusu maamuzi ya CAS kwa Rufaa ya Atletico Madrid.