Thursday, December 15, 2016

KLABU ULAYA ZAPINGA FAINALI KOMBE LA DUNIA KUWA TIMU 48

CHAMA kinachowakilisha Klabu kubwa Barani Ulaya kimeupinga mpango wa FIFA wa kuzipanua Fainali za Kombe la Dunia.
Mapema Mwezi huu Rais wa FIFA Gianni Infantino alipendekeza Fainali hizo ziwe na Timu 48 zitakazounda Makundi 16 ya Timu Tatu Tatu.
Lakini, European Club Association (ECA), Chama Cha Klabu Ulaya, kimetamka namba ya Gemu zinazochezwa kila Mwaka tayari zipo juu mno kwa kiwango ambacho hakikubaliki.
Mwenyekiti wa ECA, Karl-Heinz Rummenigge, ameeleza: "Tunaishauri FIFA isiongeze idadi ya Timu kwenye Fainali!"
Baraza la FIFA litafanya Kikao Januari 9 ili kujadili pendekezo la Rais wao.
Mara ya mwisho kwa Timu kuongezwa kwenye Fainali za Kombe la Dunia ilikuwa Mwaka 1998 kutoka Timu 24 na kufikia Timu 32.
Hata hivyo, inategemewa nyongeza ya Timu kuwa 48 haitakuwa mapema kabla ya Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2026.
Rummenigge ameonya: "Lazima tutilie mkazo mchezo wenyewe. Siasa na Biashara visipewe umuhimu kwenye Soka!"
ECA inawakilisha Vilabu zaidi ya 200 huko Ulaya ikiwa ni pamoja na Real Madrid, Barcelona, Juventus, Bayern Munich, Manchester United and Chelsea.