Friday, January 27, 2017

BEKI SUNDERLAND PATRICK APIMWA AFYA KUJIUNGA NA PALACE

BEKI wa Sunderland Patrick van Aanholt anafanyiwa upimwaji Afya yake huko Crystal Palace baada Klabu hizo mbili kuafikiana Dili inayotegemewa kufikia Pauni Milioni 14.
Beki huyo wa Kimataifa wa Netherlands mwenye Miaka 26 ataungana tena na Bosi wa Palace Sam Allardyce ambae walikuwa nae wote Sunderland.
Van Aanholt alianza kuchezea Chelsea lakini akapelekwa kucheza nje kwa Mkopo kewenye Klabu 5 na hatimae kusaini Mkataba wa kudumu na Sunderland Mwaka 2014 na kuichezea Mechi 95.

Big Sam, kama anavyojulikana Meneja wa Palace, amedokeza kuwa wapo kwenye mipango ya kusaini Wachezaji wengine wapya kabla Dirisha la Uhamisho kufungwa Januari 31 huku akidokeza hawajapokea Ofa yeyote ya Mchezaji yao yeyote kutakiwa na Klabu nyingine.

Ameeleza: “Zipo dili kadhaa lakini hazijakamilika.”
Van Aanholt amekuwa Mchezaji wa pili kusainiwa na Allardyce tangu atue Palace Mwezi uliopita kuchukua nafasi ya Alan Pardew.

Mwingine aliesainiwa na Big Sam ni Jeffrey Schlupp kutoka kwa Mabingwa wa England Leicester City kwa Dau la Pauni Milioni 13.