Friday, January 6, 2017

HULL CITY WAMCHAGUA MARCO SILVA KUWA MENEJA WAO MPYA, KAZI YAKE KUBWA KUITOA MKIANI!


Marco Silva, Raia wa Miaka 39 kutoka Ureno, ameteuliwa kuwa Meneja Mpya wa Hull City kuchukua nafasi ya Mike Phelan ambae alitimuliwa Jumanne iliyopita kufuatia matokeo mabovu yaliyoiacha Klabu hiyo ikiwa mkiani mwa EPL, Ligi Kuu England.

Hull City wapo Nafasi ya 20, ya mwisho kabisa, wakiwa Pointi 3 nyuma ya Timu ya 17 ambayo ndio nafasi salama kwenye EPL.
Silva alieanza Ukocha Mwaka 2011 akiwa na Klabu ya Daraja la Pili Estoril na kuipandisha Daraja na kisha Mwaka 2014 kuhamia Sporting Lisbon huko Ureno ambako aliiwezesha kutwaa Kombe la Ureno lakini akatimuliwa Juni 2015 ikiwa ni Siku 4 tu baada ya kutwaa Kombe hilo kwa madai ya kutovaa Sutu rasmi ya Klabu kwenye mojawapo ya Mechi zao.

Mwezi Julai 2015, Silva akajiunga na Klabu ya Ugiriki na kuiwezesha kucheza Mechi 17 za ushindi mfululizo na pia kuitwanga Arsenal 3-2 Uwanjani Emirates, London kwenye Mechi ya UEFA CHAMPIONS LIGI.

Baada ya kuipa Ubingwa wa Ugiriki, Silva akaamua kuondoka Olympiacos mwishoni mwa Msimu uliopita na tangu wakati huo alikuwa hana kibarua.