Friday, January 27, 2017

MEMPHIS DEPAY ASEMA HANA TATIZO NA MOURINHO, AMSEMA KUWA NI MTU SAFI

MCHEZAJI WA UHOLANZI Memphis Depay amesema hakuwa na uhusiano mbaya na Jose Mourinho licha ya kucheza kwa nadra chini yake.
Depay, mwenye Miaka 22, aliiihama Man United Wiki iliyopita na kujiunga na Lyon ya France baada ya kukosa namba kwenye Kikosi cha Mourinho.
Depay alicheza Dakika 20 tu za Mechi za EPL, Ligi Kuu England, Msimu huu na kuuzwa kwa Lyon Wiki iliyopita kwa Dau la Pauni Milioni 21.7 kwa Mkataba ambao una Kipengele cha Man United kumnunua tena ikiwa atatoswa huko Lyon.
Alipoondoka, Jose Mourinho, aliweka wazi milango kurejea tena kwa Depay kwa vile si ‘Mchezaji mbaya’.
Nae Depay, akiongea na OL TV na kuonyesha hana kinyongo kabisa na Mourinho kuhusu kuuzwa kwake, alitamka: “Maneno yake yalikuwa ni mazuri. Kule Manchester nilifanya bidii lakini nataka kucheza kila Mechi. Hatukuwa na uhusiano mbaya!”

Aliongeza: “Ni Kocha mzuri na Mtu mwema!”

Wikiendi iliyopita, Depay aliichezea Mechi yake ya kwanza Lyon akiingizwa kutoka Benchi na Timu yake kuichapa Marseille 3-1.

Depay, ambae huichezea Timu ya Taifa ya Netherlands, amefunga Bao 7 kwa Man United katika Mechi zake 53 alizocheza tangu ajiunge kutoka PSV Eindhoven Mei 2015 kwa Dau la Pauni Milioni 25.

Msimu huu, Depay ameichezea Man United Mechi 8 tu lakini tangu Oktoba amecheza Dakika 8 tu.

Katika kipindi hiki cha Dirisha la Uhamisho la Januari, Depay amekuwa Mchezaji wa Pili kuuzwa na Man United na mwingine ni Morgan Schneiderlin alieuzwa kwa Everton Januari 12 kwa Ada ya Pauni Milioni 24.