Wednesday, January 11, 2017

MORGAN SCHNEIDERLIN KUHAMA MAN UNITED KWENDA EVERTON, ADA YAKUBALIWA YA £24m

HABARI toka England zimebaini kuwa Klabu za Manchester United na Everton zimeafikiana Ada ya Uhamisho ya Pauni Milioni 22 kwa Kiungo Morgan Schneiderlin.
Schneiderlin, mwenye Miaka 27, alisaini Manchester United kutoka Southampton kwa Dau la Pauni Milioni 25 Julai 2015 kwenye wakati wa himaya ya Meneja Louis van Gaal.
Kiungo huyo wa Kimataifa wa France ameichezea Man United Mechi 47 lakini tangu ujio wa Jose Mourinho Msimu huu amecheza Mechi 8 tu na 3 zikiwa za EPL, Ligi Kuu England.
Mara Jana baada ya Man United kuifunga Hull City 2-0 katika Mechi ya Kwanza ya Nusu Fainali ya EFL CUP, Mourinho aligusia Uhamisho wa Schneiderlin na kueleza kuwa Makamu Mwenyekiti Mtendaji Ed Woodward alimweleza kuwa Mchezaji huyo anakaribia kuhama.
Mourinho alisema: "Nasikitika na nina furaha, nasikitika kwa sababu nampenda na angeweza kutusaidia kinamna lakini nina furaha kwa sababu hili ndio alilitaka, anataka kucheza kila Mechi na kuwa muhimu kwenye Timu!"
Ikiwa Uhamisho huu wa Schneiderlin utakamilika, Mchezaji huyo ataungana tena na Meneja Ronald Koeman huko Goodison Park baada ya kuwa wote kwa Miaka Miwili huko Southampton.
Mbali ya Schneiderlin, Koeman pia anamtaka Mchezaji mwingine wa Man United, Memphis Depay, atue Everton.
Lakini kwa Depay, Everton huenda wakaingia mvutano na Klabu nyingine za Ulaya zinazomtaka.
Depay, mwenye Miaka 22, alijiunga Man United Mei 2015 kwa Dau la Pauni Milioni 25 kutoka PSV Eindhoven ya Uholanzi.