Saturday, January 28, 2017

PAPY DJILOBODJI AFUNGIWA MECHI 4 KWA KUCHEZA RAFU UWANJANI

Beki wa Sunderland Papy Djilobodji amefungiwa Mechi 4 baada ya kukutwa na hatia ya kucheza kwa fujo.
Beki huyo mwenye Miaka 28 alipinga Kosa lake ilipodaiwa alimpiga Usoni kwa Mkono Mchezaji wa West Bromwich Albion Darren Fletcher wakati Timu yake ikichapwa 2-0 Jumamosi iliyopita kwenye Mechi ya EPL, Ligi Kuu England.

Tukio hilo halikuonwa na Waamuzi wa Mechi hiyo na kupitiwa na Jopo Huru ambalo sasa limeridhika ni Kosa lililostahili Kadi Nyekundu.

Papy Djilobodji, Mchezaji kutoka Senegal, atafungiwa Mechi 4 badala ya 3 kwa vile Novemba 19 pia alitolewa nje kwa Kadi Nyekundu kwenye Mechi ya Sunderland na Hull City.

Mchezaji huyo wa zamani wa Chelsea sasa atazikosa Mechi za Sunderland dhidi ya Tottenham hapo Januari 31 ikichezwa Nyumbani, na nyingine ni na Crystal Palace, Ugenini, Southampton, Nyumbani, na Everton, Ugenini.

Kukosekana huku kwa Papy Djilobodji ni pigo kwa Sunderland ambao wako mkiani mwa EPL.