Monday, January 2, 2017

RATIBA - EPL KUENDELEA TENA HII LEO, WEST HAM vs MAN UNITED, CITY v BURNLEY

Manchester United wanatua huko London Stadium Jijini London kucheza na Timu ngumu West Ham katika Mechi ya Ligi hiyo wakiwa kwenye wimbi tamu la ushindi wa Mechi 5 mfululizo na kutofungwa katika Mechi zao 12 zilizopita.
Leo, Jose Mourinho, Meneja wa Man United, anataka kuuanza Mwaka Mpya 2017 kwa mguu mzuri kwa kusaka ushindi dhidi ya West Ham ambayo Msimu uliopita kwenye Mechi kama hii ya EPL kwenye Uwanja wao wa zamani Upton Park walishinda 3-2.

Lakini Msimu huu, Timu hizi zimeshakumbana mara 2 na Man United kutoka 1-1 na West Ham, chini ya Meneja Slaven Bilic, kwenye EPL na Siku 4 baadae kupambana kwenye Robo Fainali ya EFL CUP na Man United kuibuka kidedea kwa Bao 4-1.

Kwenye Mechi hii, Man United itamkosa Beki wao mahiri Eric Bailly ambae Jana aliondoka Kikosini kwenda kujiunga na Timu ya Taifa ya Ivory Coast kwa ajili ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2017.

Wengine wa Man United ambao hawatakuwepo ni Majeruhi Luke Shaw na wenye hatihati kucheza ni Kepteni Wayne Rooney mwenye maumivu ya Paja na Michael Carrick ambae alikuwa Mgonjwa.

Kwa upande wa West Ham, wana Wachezaji kadhaa ambao ni Majeruhi na hao ni Diafra Sakho, Arthur Masuaku, Alvaro Arbeloa na Gokhan Tore huku wenye hatihati ni Nahodha wao Mark Noble alieumizwa Juzi kwenye Mechi yao na Leicester na kulazimika kubadilishwa na pia wengine wenye hatihati ni Daniel Amartey, Byram na Zaza.

Licha ya upungufu huo, West Ham wameibuka upya hasa baada ya kurejea Kikosini mwao kwa Majeruhi Andy Carroll na Andre Ayew lakini Man United ya sasa, iliyofufuka upya baada ya kucharazwa na Chelsea Mwezi Oktoba si mchezo.

Kimsimamo kwenye EPL, Man United wapo Nafasi ya 6 wakiwa na Pointi 36 na West Ham wapo Nafasi 12 wakiwa na Pointi 22 huku zote zikiwa zimecheza Mechi 19 kila mmoja.

 
EPL – Ligi Kuu England
RATIBA
Jumatatu Januari 2

15:30 Middlesbrough v Leicester City
18:00 Everton v Southampton
18:00 Manchester City v Burnley
18:00 Sunderland v Liverpool
18:00 West Bromwich Albion v Hull City
20:15 West Ham United v Manchester United