Friday, January 27, 2017

REFA JON MOSS ANA JOSE MOURINHO WAANGALIA TENA!

Kwa mara nyingine tena Refa Jon Moss amemkwaruza Meneja wa Manchester United Jose Mourinho baada ya maamuzi yake kwenye Mechi ya Pili ya Nusu Fainali ya EFL CUP hapo Jana kumkera Mreno huyo wakati Hull City ikiifunga Man United 2-1.

Licha ya kipigo hicho, Man United imetinga Fainali ya EFL CUP baada ya kuifunga Hull City 2-0 katika Mechi ya kwanza na hivyo kusonga kwa Jumla ya Mabao 3-2 na Fainali itakumbana na Southampton hapo Februari 26 huko Wembley Jijini London.
Wakiwa kwenye wimbi la kutofungwa Mechi 17, Man United Jana huko KCOM Stadium walijikuta wako nyuma kwa Bao 1-0 baada ya Refa Jon Moss kutoa Penati kwa Hull City na Tom Huddlestone kufunga.
Penati hiyo ilizua utata na hata kuleta Mjadala mkali kwa Wachambuzi wa Soka huko England.
Man United walisawazisha Bao hilo la Dakika ya 35 kwa Bao la Dakika ya 66 la Paul Pogba lakini Hull wakafunga Bao la Pili Dakika ya 85 kupitia Oumar Niasse.
Kwenye Mechi hiyo, mara 3 Man united walilia kupewa Penati na Refa Jon Moss kupeta tu na ya wazi kati ya zote ni pale Chris Smalling aliposukumwa ndani ya Boksi na Tom Huddlestone.
Akihojiwa baada ya Mechi hiyo, Mourinho alionyesha kukerwa na Refa Jon Moss alieamua Marcos Rojo alimsukuma Harry Maguire na kutoa Penati.
Mourinho alieleza: “Sikuona Penati. Ujumbe ni Wachezaji wetu kusherehekea tumetinga Fainali! Sitaki kuzungumzia Penati!”
Mourinho na Historia yake na Refa Jon Moss:
-Mwezi Novemba Mwaka Jana Refa Jon Moss alimtoa Uwanjani Jose Mourinho kwenye Mechi ya Man United na West Ham kwa kuipiga Teke Chupa ya Maji na akapigwa Faini na Kufungiwa kutokaa Benchi.
-Akiwa Meneja wa Chelsea, Mourinho alifungiwa kutokanyaga Uwanjani baada ya kumtukana Refa Jon Moss kwenye Mechi na West Ham na juu yake kupigwa Faini ya Pauni 40,000.

Nae Mchezaji wa zamani wa Manchester United Phil Neville alimponda Refa Jon Moss kwa kutoa hiyo Penati.

Alisema: “Kwanza nilidhani Phil Jones kamchezea Faulo Oumar Niasse nilipoangalia tena nikaona na Rojo. Ilikuwa ni Rojo kwa Harry Maguire lakini haikustahili Penati. Refa Jon Moss alikuwa kwenye nafasi nzuri kuona. Haikuwa Penati na ni uamuzi mbovu kabisa!”