Friday, January 13, 2017

TUZO EPL: MCHEZAJI BORA IBRAHIMOVIC, GOLI BORA HENRIKH MKHITARYAN

Zlatan Ibrahimovic ametwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa EPL, Ligi Kuu England, kwa Mwezi Desemba na mwenzake wa Manchester United Henrikh Mkhitaryan kuzoa ile ya Goli Bora.
Ibrahimovic, Mchezaji kutoka Sweden mwenye Miaka 35, alifunga Bao 5 Mwezi Desemba na sasa ana Jumla ya Mabao 18 tangu ajiunge na Man United mwanzoni mwa Msimu.

Desemba alifungua akaunti yake kwa Bao dhidi ya Everton huko Goodison Park na kisha kupiga Bao la ushindi kule Selhurst Park walipoicharanga Crystal Palace 2-1.
The Hawthorns ilishuhudia Ibrahimovic akipiga 2 wakati Man United inaipiga West Bromwich Albion 2-0 na kuifunga Sunderland 1 Siku ya Boksing Dei.
Pia, Ibrahimovic alifunga wakati Man United inaibwaga Zorya Luhansk 2-0 kwenye UEFA EUROPA LIGI huko Ukraine.

Tuzo hii kwa Ibrahimovic inafuatia zile za Raheem Sterling wa Manchester City, Son Heung-min wa Tottenham Hotspur na Wawili wa Chelsea Eden Hazard na Diego Costa kwa Msimu huu.

Tuzo nyingine ya Goli Bora la Mwezi imekwenda kwa Mchezaji mwingine wa Manchester United, Henrikh Mkhitaryan, kwa Bao lake la ushindi dhidi ya Sunderland ambalo limebatizwa ‘Kiki ya Nge’, Scorpion Kick.