Sunday, February 26, 2017

EFL CUP – FAINALI: LEO NI MAN UNITED vs SOUTHAMPTON, NANI KUIBUKA BINGWA WEMBLEY?

LEO Southampton, maarufu kama 'Watakatifu', wanatinga Wembley Jijini London kwenye Fainali ya Kombe la Ligi EFL CUP kucheza na Manchester United wakisaka Kombe lao la pili kubwa baada ya Mwaka 1976 kutwaa FA CUP.
Mwaka huo Watakatifu hao wakiwa Daraja la chini waliibwaga Man United 1-0 na Kutwaa FA CUP.
Lakini safari hii wanakumbana na Meneja wa Man United Jose Mourinho ambae tayari ashabeba Kombe hili mara 3 akiwa na Chelsea.
Hii Leo Southampton chini ya Meneja Claude Puel wanaweza kumtumia kwa mara ya kwanza Beki wao mpya aliewahi kuzichezea Barcelona na Juventus, Martin Caceres, mwenye Miaka 2 ambae ametua kwao Wiki iliyopita tu.
Msimu huu Man United tayari wameshabeba Ngao ya Jamii walipowafunga Mabingwa wa England Leicester City 2-1 Uwanjani Wembley Mwezi Agosti.
Ikiwa watabeba EFL CUP hili litakuwa Taji la kwanza kubwa kwa Mourinho ambae Mwezi Agosti alishaichapa Southampton 2-0 katika Mechi ya Ligi Kuu England.
Mourinho ameeleza: "Kitu muhimu ni Klabu na Msimu uliopita tulitwaa Kombe ( FA CUP) na hebu tutwae Kombe jingine Msimu huu!"

Mourinho amebainisha hali ya Kikosi
chake na kumtaja Henrikh Mkhitaryan kuwa ataikosa Fainali hii baada kuumia Jumatano wakiifunga Saint-Etienne 1-0 kwa Bao lake kwenye Mechi ya UEFA EUROPA
LIGI.
Majeruhi wengine, Kepteni Wayne Rooney na
Michael Carrick, wote amewaeleza wako fiti na pia Ander Herrera yumo baada ya
kuikosa Mechi na Saint-Etienne kwa kuwa alikuwa Kifungoni.
Kwa upande wa Southampton wao wana matumaini kuwa Kiungo wao Sofiane Boufal amepona Enka yake na atarudi dmbani.
Lakini watawakosa Majeruhi wao wa muda mrefu Charlie Austin, Virgil van Dijk, Jeremy Pied, Matt Targett na Alex McCarthy.
Mechi hii ya Leo itachezeshwa na Refa Andre Marriner mwenye Miaka 46 akisaidiwa na Richard West na Stuart Burt wakati Kevin Friend akiwa Refa wa Akiba.
Marriner alianza kuchezesha Mechi za EPL, Ligi Kuu England, kuanzia 2004 na 2013 kuchezesha Fainali ya FA CUP kati ya Man City na Wigan Athletic.
Msimu huu, Refa huyo ameshatoa Kadi za Njano 92 na Kadi Nyekundu 5 katika Gemu 24 alizosimamia lakini Kadi Nyekundu 3 kati ya hizo 5 zilitolewa katika Mechi moja ya EUROPA LIGI kati ya Panathinaikos ya Greece na Ajax ya Netherlands.
Bingwa wa EFL CUP huiwakilisha England kwenye UEFA EUROPA LIGI akianzia hatua ya Makundi.