Friday, February 10, 2017

HARRY KANE, ZLATAN IBRAHIMOVIC, ROMELU LUKAKU, DIEGO COSTA, ALEXIS SANCHEZ NANI KUZOA BUTI YA DHAHABU?

EPL, Ligi Kuu England, polepole inaelekea tamati yake ifikapo Mei na mbio za Ubingwa zinajionyesha wazi, wale wa hatarini kushuka Daraja wanachomoza na sasa wale Wachezaji wanaogombea Buti ya Dhahabu likiwa ndio Taji la Mfungaji Bora wa Msimu nao wanajibagua.
Swali kubwa miongoni mwa Wadau na Wachambuzi wa Soka hilo la England ni Je nani ataibuka na kuzoa Buti ya Dhahabu Msimu huu?
Wikiendi iliyopita, Straika wa Everton Romelu Lukaku aliwatambuka wenzake kwa kupiga Bao 4 wakiifunga Bournemouth na kushika hatamu.
Sasa Lukaku ana Bao 16 kwa Mechi 24 za Ligi akiwapita Alexis Sanchez, Diego Costa na Zlatan Ibrahimovic ambao wana Bao 15 kila mmoja.
Lakini Wachambuzi huko England hawampi Lukaku nafasi ya kuibuka kidedea na badala yake wengi wameng’ang’ana kwa Straika wa Tottenham Harry Kane mwenye Bao 14 kwa vile tu Msimu uliopita alimbwaga Jamie Vardy wa Mabingwa Leicester City kwa kufunga Bao 25.

Sababu kubwa ya ‘kumkana’ Lukaku, mwenye Miaka 23, ni kuwa hajawahi kufunga zaidi ya Bao 17 katika Msimu mmoja.
Wengi wengine wa Wachambuzi hao wako kwa upande wa Straika wa Manchester United Zlatan Ibrahimovic Mkongwe wa Miaka 35 mwenye Bao za Ligi 15 licha ya Mwezi Septemba kucheza Mechi 6 za Ligi bila kufunga lakini bomba likafunguka na kupiga Bao 9 katika Mechi 12 zilizopita za Ligi.

Yupo pia Diego Costa wa Vinara Chelsea mwenye Bao 15 ingawa sasa yupo kwenye ukame kwa kufunga Bao 1 tu tangu ‘akosane’ na Meneja Antonio Conte na kutupwa nje ya Kikosi licha ya kurejea Kikosini na pia kukosa Penati Wiki iliyopita walipotoka Sare 1-1 huko Anfield na Liverpool.
Pia hajasahaulika Mtu mkuu wa Arsenal kutoka Chile, Alexis Sanchez, ambae ana Bao 15 na ambae Mwezi Desemba alioongoza safu ya Ufungaji Bora akiwa na Bao 12 lakini tangu wakati huo amefunga Bao 3 tu katika Mechi 8 na kupitwa na Mastraika wengine.

Straika wa Timu iliyo hatarini kushuka Daraja Sunderland, Jermaine Defoe, nae yumo mbioni akiwa na Bao 14 kati ya 24 walizofunga Timu yake Msimu huu.
Pia yupo Straika wa Man City, Sergio Aguero, mwenye Bao 11 lakini yupo hatarini kukosa namba baada ya kupigwa Benchi kwa Mechi mbili zilizopita kufuatia ujio wa Straika hatari wa Brazil Gabriel Jesus.