Saturday, February 4, 2017

MKUU WA ZAMANI WA MAREFA AKIRI - MOURINHO HATENDEWI HAKI NA MAREFA ENGLAND

KEITH HACKETT, Refa na Mkuu wa zamani wa PGMOL (Professional Game Match Officials Limited), Kampuni inayosimamia Marefa wa EPL, Ligi Kuu England, ameungana na Jose Mourinho kwenye msimamo kuwa Meneja huyo wa Manchester United hatendewi haki na Marefa.
Hackett amebainisha kuwa Sheria hutafsiriwa tofauti kwa Mourinho ukilinganisha na Mameneja wengine na adhabu anazopewa pia huwa tofauti na wengine.
Hackett amenyooshea kidole adhabu ya Wenger ya kufungiwa Mechi 4 kutokaa Benchi kwa kumsukuma Refa wa Akiba wakati Mourinho alifungiwa kutokanyaga kabisa Uwanjani kwa kumpandishia tu Refa.
Hackett pia alisema kitendo alichofanya Jurgen Klopp cha kumtolea ukali Refa wa Akiba Majuzi wakati Timu yake ikitoka 1-1 na Chelsea huko Anfield na kutofanywa chochote angekuwa Mourinho angetolewa nje na kufuata Kifungo juu.

Hackett amesema kutofuatwa Sheria kikamilifu na kutumika kufuatana na nani Mkosaji kunaleta dhuluma ya haki.
Majuzi, Meneja wa Man United Jose Mourinho alilalamika na kudai yeye anaamuliwa kwa Sheria tofauti ukilinganisha na Mameneja wengine wa EPL.

Akiongea baada ya Mechi na Hull City, Mourinho alichukizwa na Refa Mike Jones kwa kushindwa kuwadhibiti Hull waliokuwa wakipoteza muda mno ili kulinda Sare yao na Mreno huyo kuongea na Refa wa Akiba.
Mourinho ameeleza: "Mnajua wazi mie niko tofauti. Sheria kwangu zipo tofauti."
Aliongeza: "Jana Refa wa Akiba alimwambia Meneja: 'Nafurahia sana msisimko wako'. Leo mie naambiwa kaa chini au tutakutoa Uwanjani!"

Msimu huu tayari Mourinho ameshatwangwa Vifungo Viwili kutokana na kuongea kuhusu Refa na pia kupiga Teke Chupa ya Maji akiwa Uwanjani.