Thursday, March 16, 2017

AHMAD AMBWAGA HAYATOU CAF, ZANZIBAR SASA MWANACHAMA WA 55 WA CAF

KIONGOZI wa Chama cha Soka cha Madagascar anaetambulika kwa Jina moja tu, Ahmad, amechaguliwa kuwa Rais mpya wa Shirikisho la Soka Afrika CAF na rasmi kuimaliza himaya ya Issa Hayatou aliedumu Miaka 29.

Ahmad alizoa Kura 34 kati ya 54 kwenye Uchaguzi uliofanyika hii Leo huko Addis Ababa Mji Mkuu wa Ethiopia.

Mabadiliko hayo ni ya kwanza tangu Hayatou ashika hatamu Mwaka 1988 na Ahmad anakuwa Rais wa 7 wa CAF katika enzi ya Miaka 60 ya Shirikisho hilo.

Mara baada ya kuchaguliwa, Ahmad, mwenye Miaka 57, alishindwa kuongea lolote kwa kukabwa na furaha huku Wajumbe wakimbeba juu kwa juu kwa furaha.

ZANZIBAR SASA MWANACHAMA WA 55 WA CAF
Mapema Leo, Zanzibar imeingizwa rasmi kama Mwanachama wa 55 kufuatia Kikao cha 39 cha Mkutano Mkuu wa CAF.
Mapendekezo ya kukubaliwa Zanzibar kama Mwanachama kamili wa CAF yalipendekezwa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi, na kupitishwa kwa kauli moja na Wanachama 54 wa CAF.

Awali Zanzibar ilikuwa ikiruhusiwa kucheza Mashindano ya Klabu Afrika lakini kwenye yale ya Timu za Taifa ilibidi ishiriki pamoja na Tanzania Bara kama Nchi moja Tanzania.

Baada ya hatua hii ya kupata Uanachama kamili, sasa Zanzibar ipo huru kuwakilishwa na Timu yake ya Taifa na pia kupata Misaada ya Fedha moja kwa moja kutoka CAF na FIFA badala ya kupitishwa TFF.