Wednesday, March 22, 2017

ARSENE WENGER ARUKA TETESI ZA KWENDA PSG, HAKUNA KITU KAMA HICHO!

Arsene Wenger amezikanusha habari kuwa amepewa Mkataba kujiunga na Mabingwa wa Nchini kwao France, Paris Saint-Germain.
Wenger, mwenye Miaka 67, anamaliza Mkataba wake na Arsenal mwishoni mwa Msimu huu lakini tayari Klabu hiyo ishamwekea Mezani Mkataba Mpya wa Miaka Miwili na yeye Juzi, mara baada ya kutandikwa 3-1 na West Bromwich Albion huko The Hawthorns, kutamka tayari ashaamua nini hatima yake na uamuzi huo utakuwa bayana hivi karibuni.
Kipigo hicho cha Arsenal ni chao cha 4 katika Mechi zao 5 za mwisho za EPL, Ligi Kuu England na kimewashusha hadi Nafasi ya 6.
Hali hiyo imewagawanya mno Mashabiki wa Arsenal na kumekuwa na Maandamano ya Makundi Mawili kati yao, moja likimpinga na jingine kumsapoti.

Hivi karibuni Wenger alikaririwa akisema kuwa ikiwa ataondoka Arsenal basi atatua Klabu nyingine kuendelea na kazi na PSG, Klabu ya Nchini kwao na Tajiri, inaonekana ni muafaka kwake hasa baada ya Meneja wao Msimu huu, Unai Emery, kuonekana kuyumba.
Lakini Wenger hii Leo amekanusha uvumi huo kwa kutamka: “Ni uvumi wa uongo, ni kile kinachoitwa ‘Habari Feki’! Naikanusha rasmi, si kweli!”
Mbali ya kuzorota hivi karibuni, na hasa kubamizwa Jumla ya Bao 10-2 na Bayern Munich katika Mechi 2 na kutupwa nje ya UCL, UEFA CHAMPIONS LIGI, Wachambuzi huko England wamesisitiza Wenger atasaini Mkataba mpya na kubaki Arsenal.

Pengine tamko la kubakia huko Emirates linasubiri nini kitajiri kwa matokeo ya Uwanjani ya Mwezi Aprili ambao wanauanza kwa mtanange mkali wa EPL hapo Aprili 2 wakiwa Nyumbani kuwavaa Man City ambao pia watapambana nao tena huko Wembley Stadium kwenye Nusu Fainali ya FA CUP hapo Aprili 23.