Thursday, March 16, 2017

BARCELONA, BAYERN, REAL, BUFFON WAIHOFIA LEICESTER ULAYA, DROO ROBO FAINALI IJUMAA!

KIPA wa Juventus Gianluigi Buffon hataki wao wapangiwe Leicester City kwenye Mechi za Robo Fainali ya UCL, UEFA CHAMPIONS LIGI.
Jana Leicester na Juve zilitinga Robo Fainali za UCL na kuungana na Mabingwa Watetezi Real Madrid, Barcelona, Bayern Munich na Borussia Dortmund zilizofuzu Wiki iliyopita.
Timu mbili za mwisho kutinga Robo Fainali zitapatika Leo baada ya Mechi 2 kati ya AS Monaco na Man City na ile ya Atletico Madrid na Bayer Leverkusen.
Licha ya kuwepo Vigogo wote hao, Buffon, mwenye Miaka 39, anataka kuwakwepa Leicester ambao Msimu uliopita walishangaza wengi kwa kutwaa Ubingwa wa England kwa mara ya kwanza katika Historia yao ya Miaka 100.
Akiongea na Tovuti ya Klabu yake Juventus, Buffon ameeleza: "Napenda kuwakwepa Leicester. Ni Timu hatari. Sasa wapo sawa na wanaweza kukudhuru ukiwashambulia. Ukicheza nao wewe ndio unapoteza kila kitu!"
Juventus hawajawahi kuvaana na Leicester katika Mashindano yeyote lakini wameshawahi kukutana na Timu nyingine za England ambazo ni Fulham, Manchester City na Chelsea waliocheza nao mara 2.
Droo ya kupanga Mechi za Robo Fainali itafanyika Ijumaa na hii ni Droo huru ikimaanisha yeyote anaweza kukutana na yeyote bila kubagua kama wanatoka Nchi moja.