Wednesday, March 8, 2017

IBRAHIMOVIC AFUNGIWA MECHI TATU(3) KUIKOSA CHELSEA JUMATATU!

Zlatan Ibrahimovic atatumikia Kifungo cha Mechi 3 baada ya kukiri Shitaka la FA, Chama cha Soka England, la mchezo wa fujo.

Straika huyo wa Manchester United alishitakiwa kwa Kosa la Kumpiga Kiwiko Beki wa Bournemouth RTyrone Mings Jumamosi iliyopita zilipotoka Sare 1-1 katika Mechi ya EPL, Ligi Kuu England.

Baada ya Mechi hiyo, Ibrahimovic alikataa kuwa hakufanya kusudi kumpiga Kiwiko Mings lakini baada ya kufunguliwa Mashitaka akakiri Kosa ili kuepuka Kifungo cha muda mrefu baadae.

Adhabu hii ya kufungiwa Mechi 3 itamfanya azikose Mechi ya Robo Fainali ya FA CUP dhidi ya Chelsea na Mechi za Ligi dhidi ya Middlesbrough na West Bromwich Albion.

Nae Mings pia alifunguliwa Mashitaka kama Ibrahimovic kwa kumtimba Kichwani Straika huyo wa Man United na FA kudai Kosa lake linastahili Kifungo cha zaidi ya Mechi 3 lakini Beki huyo akaamua kukata Rufaa kupinga hayo.