Tuesday, March 28, 2017

KIMATAIFA KIRAFIKI: TAIFA STARS 2-1 BURUNDI, MBARAKA YUSUPH AIPA USHINDI STARS

Tanzania, maarufu kama Taifa Stars, Leo imeiwasha Burundi, maarufu kama Intamba Murugamba, Bao 2-1 kwenye Mechi ya Kimataifa ya Kirafiki Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Wakicheza bila ya Nahodha wao Mbwana Samatta, Stars waliongoza 1-0 hadi Mapumziko kwa Bao la Siimon Msuva aliefunga Dakika ya 22.
Burundi walisawazisha Bao hilo Dakika ya 53 kwa Bao la Mchezaji wa Simba ya Dar es Salaam Laudit Mavugo lakini Chipukizi kutoka Kagera Stars, alietokea Benchi, Mbaraka Yussuf, aliipa ushindi Taifa Stars baada ya kuinasa Pasi ya Msuva na kusonga mbele akiachia Shuti lilopiga Mwamba na yeye mwenyewe kumalizia Mpira uliorudi hadi Wavuni katika Dakika ya 77.
Huu ni ushindi wa Pili kwa Stars kwenye Mechi ya Pili ya Kocha Mpya Salum Mayanga, anaesaidiwa na Patrick Mwangata, baada ya Majuzi Jumamosi kuiwasha Botswana, maarufu kama The Zebras, ‘Pundamilia’, Bao 2-0 pia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Bao zote kupigwa na Samatta.
Leo Samatta hakucheza Mechi hii baada ya kulazimika kurudi Klabuni kwake KRC Genk huko Belgium.

VIKOSI:
TANZANIA: Deo Munishi ‘Dida’, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Salim Mbonde, Himid Mao, Muzamil Yassin [Jonas Mkude], Salum Abubakar [Said Ndemla], Ibrahim Ajib [Shiza Kichuya], Farid Mussa [Mbaraka Yussu], Simon Msuva

BURUNDI: Jonathan Nahimana, Gael Duhayindavya, Rashid Harerimana, Omary Moussa, David Nshirimimana [Eric Ndoyirobija], Youssouf Ndayishimiye, Tresor Ndikumana, Jean Ndarusanze [Franck Barirengako], Laudit Mavugo, Kiza Fataki [Moustapha Selemani], Djuma Nzeyimana [Sudi Ntirwaza]

REFA: Israel Mujuni Nkongo