Wednesday, March 22, 2017

KLABU YA SIMBA YAOMBWA KUTANGAZA TANZANITE

Kampuni ya Madini ya Tanzanite One imeuomba uongozi wa timu ya soka ya Simba kuyatangaza madini ya Tanzanite ambayo duniani yanapatikana pekee mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ili yaweze kupata soko zaidi.

Mkurugenzi wa kampuni ya TanzaniteOne Hussein Gonga akizungumza juzi baada ya viongozi na wachezaji wa timu hiyo kutembelea migodi alisema Simba ina uwezo mkubwa wa kuitangaza Tanzanite.

“Kupitia ninyi tutapata nafasi kubwa ya kujitangaza kwani Simba
ni timu kubwa na ina marafiki wengi ndani ya nchi na nje ya nchi na naamini kampeni hii itakuwa na mafanikio makubwa,” alisema Gonga.
Pia alisema wachezaji na viongozi wa timu hiyo kwa nafasi yao wana uwezo mkubwa wa kuyatangaza mafanikio yaliyopatikana kupitia madini ya Tanzanite, ndani na nje ya nchi ya Tanzania.

Mkurugenzi mwenza wa kampuni ya TanzaniteOne Faisal Shabhai
akizungumza akiwa Mazubu Grand Hotel mji mdogo wa Mirerani ambapo timu ya Simba ililala alisema ziara hiyo itakuwa na mafanikio makubwa.

Shabhai alisema kupitia nafasi hiyo timu ya Simba itayatangaza vya kutosha madini ya Tanzanite ambayo kwa namna ya pekee imeyabadili maisha ya wananchi wa eneo hilo na serikali kupata kodi yake.

Makamu wa Rais wa Simba Jofrey Kaburu alisema ziara hiyo itawanufaisha viongozi na wachezaji ambao walikuwa hawajawahi kutembelea migodi na kujionea madini ya Tanzanite yaliyovyo.

Kaburu alisema Tanzanite ni kitu muhimu kwenye jamii na
watawafahamisha watanzania na kuwaelimisha madini hayo kwa hapa duniani yanapatikana kuwa Mirerani pekee hivyo ni jambo la kujivunia.

“Mji wa Mirerani hivi sasa umeendelea tofauti na awali tulivyokuja
miaka mitano iliyopita kwani tumeona maendele mengiikiwemo Mazuru Grand Hotel ambapo timu yetu ilifikia,” alisema Kaburu.

Alitoa pongezi kwa uongozi wa kampuni ya TanzaniteOne ambayo
inamilikiwa na wazawa kwa kutoa ajira kwa wananchi na kuendesha ipasavyo mgodi huo huku ikilipa kodi kwa serikali.

Baada ya kumaliza kutembelea machimbo madini kwenye kampuni ya TanzaniteOne, timu ya Simba ilicheza mchezo wa kirafiki na timu ya Mirerani Stars kwenye uwanja wa barafu Mirerani na kushinda bao 1-0 lililofungwa na Mwinyi Kazimoto.