Tuesday, March 28, 2017

MAN CITY YADUNGWA FAINI, MORATA AITAKA CHELSEA!

Manchester City wametwangwa Faini ya £35,000 na FA, Chama cha Soka England, kutokana na Utovu wa Nidhamu wa Wachezaji wao wakati walipotoka Sare 1-1 na Liverpool hapo Machi 19 katika Mechi ya EPL, Ligi Kuu England.
City ilikiri kosa la kutodhibiti Wachezaji wao kufuatia tukio la Dakika ya 50 ya Mechi hiyo ambapo Refa Michael Oliver aliipa Penati Liverpool na Refa huyo kumpa Kadi ya Njano Gael Clichy kwa Rafu iliyozaa Penati hiyo na David Silva kwa kulalamikia Penati hiyo huku Wachezaji kadhaa wakimzonga Refa.
James Milner alifunga Penati hiyo na Sergio Aguero kuisawazishia City katika Dakika ya 69.

ALVARO MORATA AITAKA CHELSEA 
JANA zimeibuka ripoti kutoka Spain kwamba Alvaro Morata ataihama Real Madrid mwishoni mwa Msimu huu ili kuungana tena na Antonio Conte huko Chelsea.

Wawili hao walikuwa pamoja huko Italy Klabuni Juventus Msimu uliopita na kuisaidia kutwaa Ubingwa wa Serie A kabla hawajatengana kwa Morata kurejea Real na Conte kwenda Chelsea.

Lakini tangu arejee Real, Morata, mwenye Miaka 24 na ni Mchezaji wa Kimataifa wa Spain, amekuwa hana Namba ya kudumu ndani ya Kikosi cha Zinedine Zidane.

Ripoti hizo zimedai Conte ashamtonya Mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich kuhusu kumnunua Morata lakini vikwazo ni hatima za Wachezaji wao Eden Hazard na Diego Costa.

Hivi sasa Hazard anatajwa kuhamia Real huku kukiwa hamna lolote kuhusu Costa ingawa nae anavumishwa kutaka kuondoka Chelsea.