Thursday, March 16, 2017

MAN UNITED YASHITAKIWA NA FA KWA KUMZONGA REFA

Manchester United wamefunguliwa Mashitaka na FA, Chama cha Soka England, kwa kushindwa kudhibiti Wachezaji wao huko Stamford Bridge Juzi walipofungwa 1-0 na Chelsea na kutolewa nje ya FA CUP kwenye Mechi hiyo ya Robo Fainali.
Shitaka hilo linatokana na Wachezaji wa Man United kumzonga Refa Michael Oliver alipoamua kumtoa nje kwa Kadi Nyekundu Kiungo wao Ander Herrera katika Dakika ya 35.
Herrera alitolewa baada ya kupewa Kadi za Njano 2 ambazo Meneja wao Jose Mourinho amedokeza hazikustahili na pia 'kumtuhumu' Refa Oliver 'kuiwinda' Man United kwa kutoa Penati 3 na Kadi Nyekundu 1 dhidi yao Msimu huu.
Kwenye Mechi 3 za Ligi Kuu England Refa Oliver alizoichezesha Man United Msimu huu, zile walizofungwa na Watford na sare na Liverpool na Everton, zote Refa Oliver alitoa Penati dhidi yao.
FA imeipa Man United hadi Saa 3 Usiku Ijumaa kujibu Shitaka lao.
Kawaida kosa kama hili huadhibiwa kwa Faini.
Wakati huo huo Refa Michael Oliver 'amemwokoa' Beki wa Man United Marcos Rojo kukumbana na Shitaka la FA baada kuonekana akimtimba Kifuani Mchezaji wa Chelsea Eden Hazard kwenye Mechi hiyo ya. Juzi.

Imebainika Refa Oliver ameliingiza tukio hilo kwenye Ripoti yake ya Mechi na kusema alichukua hatua stahiki na hivyo kuibana FA kutofungua Mashitaka.
Laiti kama Refa Oliver asingelibaini tukio hilo kwenye Ripoti basi FA ingekuwa huru kumshitaki Rojo.