Friday, April 7, 2017

ARSENE WENGER KUBAKI EMIRATES.

MENEJA wa Arsenal Arsene Wenger Leo ametoa ishara ya kubakia kwake Klabuni hapo baada kuzungumzia mipango yao ya kabla Msimu Mpya wa 2017/18 kuanza.
Wenger, ambae Mkataba wake na Arsenal unamalizika mwishoni mwa msimu huu na tayari upo Mezani Mkataba Mpya wa Miaka Miwili, amekataa kutoboa kama ataendelea na Arsenal au atang’oka huku kukiwa na presha kutoka Kundi la Mashabiki wakitaka aondoke.
Mkataba wa Wenger, mwenye Miaka 67 na ambaye yuko Arsenal kwa Miaka 20, unaisha Juni lakini ametoa fununu za mipango yake kwa ajili ya Msimu Mpya unaoanza Agosti.
Wenger ameeleza: “Ninayo Mipango. Hiyo ndio kazi yangu kupanga.”

Alipobanwa nani atatangaza kama atabaki Arsenal, Wenger alijibu: “Klabu. Sina la kuongeza hapo. Siwezi kusema zaidi na nlichosema awali!”
Hivi karibuni Wenger alitamka kuwa ashaamua kuhusu kubaki au kuondoka Arsenal na Watu wasubiri tamko tu.

Hivi sasa Arsenal wapo Nafasi ya 5 kwenye EPL, Ligi Kuu England, na pia Nusu Fainali ya FA CUP ambako watacheza na Man City kwenye Nusu Fainali.