Monday, April 3, 2017

CONTE ACHUKIZWA NA KICHAPO CHA BAO 2-1 KUTOKA KWA CRYSTAL PALACE


KOCHA wa Chelsea Antonio Conte amesema kipigo cha kushtukiza walichokipata jana kutoka kwa Crystal Palace kwenye uwanja wa Stamford Bridge kimevuruga mambo na kufanya mbio za ubingwa kuendelea kuwa ngumu.
Vinara hao wa ligi wamekubali kipigo cha pili msimu huu katika uwanja wa nyumbani baada ya kuadhibiwa mabao 2-1 na vijana hao wa Sam Allardyce.
Ushindi wa Tottenham Hotspurs walioupata dhidi ya Burnley unamaanisha tofauti baina yao imebaki kuwa pointi saba kutoka kumi za awali.
“Kwa vyombo vya habari ni matokeo mazuri kwa sababu yana furahisha mbio za ubingwa.
“Lakini siku zote ninasema ligi inaisha ukifanya mahesabu vinginevyo unatakiwa kupambana kuhakikisha kila mchezo unashinda,” alisema Conte.
Kwa upande wake kocha wa Spurs Mauricio Pochettino amesema wachezaji wake wanaamini wanaweza kuwafikia Chelsea kileleni kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burnley.
“Ni muhimu sana kupata pointi tatu, kunatufanya tuendelee kuamini tunaweza kupambana kupata ubingwa.
“Tumeonyesha imani kubwa kuwa tunaweza kufanya vizuri. Tunajivunia kwa hilo,” alisema Pochettino.
Kocha wa Palace Sam Allardyce alisema hakuna aliyetegemea kuwa wataweza kuifunga Chelsea kwakuwa hawakuwahi kufungwa kwenye michuano yoyote uwanjani hapo tangu walipokubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Tottenham Januari 4.
“Hakuna aliyetarajia,” alisema Allardyce ambaye hajawahi kushuka daraja akiwa meneja katika klabu zinazoshiriki ligi kuu nchini Uingereza.