Thursday, April 27, 2017

DONDOO.. MANCHESTER: MANCHESTER CITY v MANCHESTER UNITED

ETIHAD, ndio Uwanja ambao Alhamisi Aprili 27 kuanzia Saa 4 Usiku utakuwa dimba la Dabi ya Jiji la Manchester kati ya Mahasimu Manchester City na Manchester United.
 
4 Bora
Hii ni Mechi ya EPL, Ligi Kuu England, ambayo inazikutanisha City walio Nafasi ya 4 na Man United ambao wako Nafasi ya 5 wakiwa Pointi 1 nyuma.
Hivyo Mechi hii ni muhimu katika zile mbio za kumaliza 4 Bora ili kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI kwani baada ya Mechi hii Timu hizi zitabakiza Mechi 5 kila mmoja.

Nini kilijiri kabla pambano hili
Jumapili Man United walicheza Ugenini kwenye EPL na kuichapa Burnley 2-0 wakati City wakipigwa 2-1 katika Dakika 120 za Mchezo na Arsenal huko Wembley katika Mechi ya Nusu Fainali ya FA CUP, kipigo ambacho kinaweza kumfanya Meneja wa City Pep Guardiola kumaliza Msimu bila Kombe lolote kwa mara ya kwanza katika Maisha yake ya Ukocha.
Hali za Timu
Man United ndio wenye athari kubwa wakiwa na mlolongo wa Majeruhi ambao ni Marcos Rojo, Zlatan Ibrahimovic, Phil Jones, Chris Smalling, Juan Mata na Paul Pogba.

JE WAJUA?
-Ikiwa Man United hawatafungwa Mechi hii na City basi wataifikia Rekodi yao ya kutofungwa Mechi 24 kwenye Ligi ya juu ambapo Msimu wa 2010/11 walienda Mechi 24.
-Hivi sasa wapo kwenye mbio za Ushindi 13 Sare 10 tangu wafungwe Oktoba Mwaka Jana na Chelsea.


Kwa City, wapo Wachezaji kadhaa wenye maumivu na hivyo kutokuwa na uhakika kama watacheza au la.

Hao ni Sergio Aguero na David Silva ambao Majuzi walilazimika kutoka walipofungwa na Arsenal na wengine ni Fernandinho pamoja na Majeruhi wao wa muda mrefu John Stones, Gabriel Jesus na Bacary Sagna.

Mechi za hivi karibuni
Msimu uliopita Man United walishinda 1-0 hapo Etihad kwa Bao la Marcus Rashford.
Msimu huu, Timu hizi zimekutana mara 2 Uwanjani Old Trafford kwa City kushinda 2-1 kwenye EPL Mwezi Septemba na Oktoba Man United kuitungua City 1-0 kwenye EFL CUP kwa Bao la Juan Mata.

FAHAMU:
-Hii Gemu ilipaswa kuchezwa Februari lakini ikaondolewa kutokana na Man United kucheza Fainali ya EFL CUP.
-Mara ya mwisho kwa Dabi ya Manchester kupigwa Alhamisi ilikuwa ni Tarehe 10 Novemba 1994 Uwanjani Old Trafford na Man United kuibuka kidedea 5-0 kwa Hetitriki ya Andrei Kanchelskis.

JOSE MOURINHO – Nini kasema:
“Ipo Pointi 1 kati ya Timu hizi kwa hiyo hali iko wazi lakini City wanacheza Ligi Kuu na sisi tupo Nusu Fainali ya UEFA EUROPA LIGI. Ndio, ni lengo kumaliza 4 Bora lakini nahisi Klabu hii inapaswa kushinda Makombe. Kwenye Ligi hatuwezi kubeba Kombe lakini EUROPA LIGI tuna nafasi Asilimia 25. Nadhani tutilie mkazo wote kwenye EUROPA LIGI!”