Thursday, April 6, 2017

FIFA LISTI UBORA DUNIANI: BRAZIL YAPANDA JUU NI NAMBARI WANI, EGYPT JUU AFRIKA, TANZANIA YAPANDA 22!

WAKATI Brazil imekamata Nambari Wani Duniani katika Listi ya Ubora Duniani iliyotolewa hii Leo na FIFA, Tanzania imechomoka kutoka Nafasi ya 157 iliyoshikilia Mwezi uliopita na kupanda Nafasi 22 juu.
Brazil imerejea kileleni kwa mara ya kwanza baada ya Miaka 6 na hili limekuja baada ya mafanikio makubwa chini ya Kocha wao Tite ambae ameshinda Mechi 9 mfululizo tangu atwae wadhifa Mwaka Jana wakifunga Bao 25 na kufungwa 2 tu.

Hivi karibuni Brazil ilishinda Mechi zake zote 2 za Kundi la Nchi za Marekani ya Kusini na kuwa Nchi ya Kwanza kufuzu kuingia Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2018 huko Russia.
Wiki iliyopita, Brazil kwanza iliifunga Uruguay 4-0 huko Montevideo na Siku 3 baadae kuichapa 3-0 Paraguay huko Sao Paolo, Brazil.

Brazil wameitoa Argentina kwenye Namba 1 ya Listi ya Ubora baada ya Argentina hivi karibuni kushinda Mechi 1 tu, walipoifunga Chile 1-0, na kisha kuchapwa 2-0 na Bolivia.
Argentina sasa wameshika Namba 2 baada kukaa kileleni kwa Miezi 12 walipowang'oa Mabingwa wa Dunia Germany ambao sasa wako Nafasi ya 3.

Katika 10 Bora Nchi pekee mpya ni Switzerland ambayo ipo wa 9 baada ya kuifunga Latvia 1-0 kwenye Mechi ya Kundi lao la Ulaya la kusaka kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2018.

Nao Vigogo Netherlands, baada ya Wiki hii kuchapwa na Bulgaria na Italy, wamezidi kuporomoka kwa Nafasi 11 na kuangukia Nafasi ya 32 ikiwa ndio Nafasi ya chini kabisa katika Historia yao.
Wengine walioporomoka mno ni Uruguay walioshuka Nafasi 6 na kuangukia Nafasi ya 15 baada Wiki hii kuchapwa na Brazil na Peru.
Wakati Egypt ndiyo Timu ya juu kabisa kwa Afrika ikishika Nafasi ya 19, Tanzania sasa ipo Nafasi ya 135 ikitokea Nafasi ya 157 baada ya kuzifunga Botswana na Burundi Nchi ambazo ziko juu yake.

FIFA LISTI YA UBORA DUNIANI – 20 BORA:
1. Brazil
2. Argentina
3. Germany
4. Chile
5. Colombia
6. France
7. Belgium
8. Portugal
9. Switzerland
10. Spain
11. Poland
12. Italy
13. Wales
14. England
15. Uruguay
16. Mexico
17. Peru
18. Croatia
19. Egypt
20. Costa Rica