Sunday, April 16, 2017

KUELEKEA EL CLASICO – REAL MADRID NA BARCELONA ZASHINDA, ZATAMBIANA!

Vinara wa La Liga walihitaji Bao la Dakika ya 90 na kuifunga Sporting Gijon 3-2 huko Estadio El Molinon kwenye Mechi ya La Liga iliyochezwa Jana.
Baadae Usiku, Barcelona nao, wakiwa kwao Nou Camp, waliifunga Real Sociedad 3-2 na kufanya Timu hizo zifukuzane kileleni mwa La Liga.
Real sasa wanaongoza La Liga wakiwa na Pointi 75 kwa Mechi 31 na Barcelona ni wa Pili wakiwa na Pointi 72 kwa Mechi 32.
Wakicheza bila Mastaa wao Cristiano Ronaldo, Gareth Bale na Karim Benzema waliopumzishwa kwa ajili ya Mechi ya Marudiano ya UEFA CHAMPIONS LIGI dhidi ya Bayern Munich itakayochezwa Santiago Bernabeu Jumanne ijayo, Real walitoka nyuma kwa Bao la Duje Cop na Isco kuwasawazishia.

Kisha Vesga akawapa tena uongozi Sporting Gijon lakini Alvaro Morata akarudisha.
Ndipo Isco tena, kwenye Dakika ya 90, kuifungia Real Bao la 3 na la ushindi.
Baadae huko Nou Camp, Barcelona waliichapa Real Sociedad 3-2 kwa Bao za Lionel Messi, Bao 2, na Paco Alcacer wakati za Sociedad zilifungwa na Samuel Umtiti, aliejifunga mwenyewe, na Xabier Pieto.

Wikiendi ijayo huko Santiago Bernabeu, ni ule mtanange mkale uliobatizwa El Clasico kati ya Real Madrid na Barcelona.