Thursday, April 27, 2017

TOKA TFF: PATA TAARIFA KAMILI SABABU ZA SIMBA KUPOKWA POINTI ZA ‘DEZO’ TOKA KWA KAGERA SUGAR!

UAMUZI WA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA HADHI ZA WACHEZAJI
Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana tarehe 23 Aprili 2017 imekamilisha mapitio ya maamuzi ya Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi (Kamati ya Masaa 72).
Baaada ya Mapitio hayo yafuatayo yamejitokeza :


I. Kamati kwa kauli moja imeona kuna Kasoro za kikanuni katika maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Uendeshaji wa Usimamizi wa Ligi kwa sababu zifuatazo:

1.Malalamiko ya Klabu ya Simba kutowasilishwa kwa wakati kwa mujibu wa kanuni 20(1) ya Kanuni za Ligi Kuu toleo la 2016 inayotaka malalamiko yoyote yanayohusiana na mchezo yawasilishwe kwa maandishi Bodi ya Ligi Kuu sio zaidi ya masaa 72 baada ya mchezo kumalizika.

2.Malalamiko hayo hayakulipiwa ada kwa mujibu wa kanuni 20(4) kinachosema ada ya malalamiko ni Shs. 300,000/= (Shilingi laki tatu). Malalamiko yatakayowasilishwa bila kulipiwa ada au baada ya muda uliowekwa hayatasikilizwa.

3.Kikao cha Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa ligi kilikosa uhalali baada ya kuwashirikisha wajumbe waalikwa ambao sio sehemu ya kamati hiyo.

Hivyo kwa msingi huo malalamiko ya Simba hayana mashiko kikanuni hivyo matokeo ya mchezo wa Kagera Sugar dhidi ya Simba Sports Club yanabakia kama yalivyokuwa awali (2-1).

Pia kamati kwa kupitia taarifa za mchezo namba 165 unaolalamikiwa wa Kagera Vs Africa Lyon kumejitokeza mapungufu mengi ya msingi kwa mujibu wa rekodi zilizopokelewa na Bodi ya Ligi na kutumika katika kikao tajwa, kwa mfano:

1- Matokeo ya mchezo referee na kamisaa walipishana, mmoja (Kamisaa) alisema matokeo ya mwisho wa mchezo yalikuwa 2-1 na Mwamuzi alisema 2-0.

2- Refa na Kamisaa wanapishana sababu ya adhabu hiyo mwamuzi anasema kumvuta mpinzani na Kamisaa anasema kumrukia mpinzani.

3- Kamisaa kutopeleka taarifa ya mchezo TFF kwa maelezo ya kukosea address ya barua pepe kwa mara ya kwanza toka awe kamisaa.

4- Bodi ya Ligi kutumia matokeo ya Kamisaa yaani 2-1, na kwa msingi huo taarifa ya refa kukosa weledi. Uzoefu unaonyesha ni rahisi kukumbuka matokeo sio kadi.

5- Utoaji taarifa wa refa kupitia address ya barua pepe ya mtu mwingine kwa maelezo yanayo pelekea kutia shaka weledi wake kuwa alipoteza simu na hivyo mabadiliko ya simu ndiyo kiini cha utumaji taarifa kupitia barua pepe ya muamuzi mwenzake kinyume na utaratibu.

6- Kutofanyika kwa kikao cha brief ya waamuzi baada ya mchezo kama ilivyo ada kwa maelezo ya mwamuzi kuwa hakukuwa na tukio.

7- Uongozi wa African Lyon kugoma kutoa ushirikiano kwa kamati juu uwepo wa kadi ya njano kwa sababu za kuogopa kuathiriwa na ushiriki wao katika suala hili.

8- Mchezo kubadilishwa tarehe na hivyo kukosekana records.

9- Ligi kusimama baada ya mchezo wa Kagera Vs Majimaji toka tarehe 4.3.2017 Mpaka tarehe 2.4.2017 ambapo Simba ilicheza na Kagera na kwa hivyo kulikuwa na muda wa kutosha kwa chombo kinachosimamia ligi kuweka rekodi sawa kupitia mfumo wa taarifa.

10-Uwepo wa rekodi zinazoonyesha maamuzi ya refa kuhusu utoaji wa kadi sio ya mwisho.

Yote hayo hapo juu yanazua maswali juu ya uwepo wa taarifa sahihi za kadi na hivyo kufanya hoja pinzani yaani BENEFIT OF DOUBT iwe IN FAVOR OF KAGERA SUGAR FC. Kwa kuwa ni rahisi kukumbuka matokeo na sio kadi.

Vilevile Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji imependekeza kupitia kwa ofisi ya Katibu Mkuu wa TFF:

1- Kuwachukulia hatua stahiki watendaji na maofisa wote ambao ama hawakuwajibika ipasavyo au kutenda kosa la kuipotosha Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi kinyume na katiba.

2- Kutoa waraka kwa waamuzi na makamisaa utakaolekeza bayana namna ya kuwasilisha taarifa kwa Bodi ya Ligi na TFF.
IMETOLEWA NA TFF