Saturday, May 20, 2017

ARSENAL – ‘VITA YA HISA’: USMANOV ATAKA ‘KUITEKA’, WASHABIKI WATAKA MWANAHISA MKUBWA STAN KROENKE, WENGER WATIMKE!

JANA ilitangazwa kuwa Mfanyabiashara kutoka Russia Alisher Usmanov ametoa Ofa ya Pauni Bilioni 1 ya kununua Hisa za Klabu ya Arsenal.
Usmanov, mwenye Miaka 63, anamiliki Hisa Asilimia 30 za Arsenal kupitia Kampuni yake Red & White Holdings na sasa anataka kununua Hisa Asilimia 67 za Klabu hiyo zinazomilikiwa na Mmarekani Stan Kroenke.
Mara baada ya kuibuka Taarifa hizo, baadhi ya Washabiki wa Arsenal wakaibukia Mitandao ya Jamii na kumtaka Stan Kroenke na Meneja wa Timu Arsene Wenger wang’oke.
Hata hivyo, inaaminika Kroenke atagoma kuuza Hisa zake.
Usmanov amekuwa Mmiliki wa Hisa za Arsenal tangu 2007 na baadae kuongeza Hisa hizo kutoka Asilimia 14.6 hadi 30 Mwaka 2016 baada ya kununua Hisa za Farhad Moshiri.

Usmanov na Kroencke hawana uhusiano mzuri na Mwezi uliopita Mrusi huyo alidai ishu za Klabu zisiwekwe mgongoni mwa Wenger pekee.

Usmanov, akiongea na Wasambaza Taarifa za Kifedha Bloomberg, alieleza: “Sidhani Kocha pekee ndie alaumiwe kwa kinachotokea Arsenal. Bodi na Mmiliki Mkuu wa Hisa [Kroencke] wana wajibu mkubwa!”

Endapo Arsenal watakosa kufuzu 4 Bora ya EPL, LIGI KUU ENGLAND, basi hawatacheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao na hilo litaathiri sana Mapato yao kwa kukosa Mamilioni ya Pauni.

Jumapili Arsenal wanamaliza EPL kwa kucheza na Everton na, ili kutinga 4 Bora, wanatakiwa washinde Mechi hiyo na kuomba Matokoeo ya Mechi za Man City na Liverpool yawe upande wao.

Ingawa Ofa hii ya Pauni Bilioni 1 itampa Faida kubwa Kroencke, Mmarekani huyo anasadikiwa kutotaka kuuza Hisa zake lakini pia imedaiwa Usmanov, ambae Utajiri wake unasadikiwa kuwa Pauni Bilioni 11.2, yupo tayari kupandisha Dau la Ofa yake.