Saturday, May 20, 2017

HERRERA AZOA TUZO YA SIR MATT BUSBY, NDIE BORA MAN UNITED 2016/17! >GOLI BORA MKHITARYAN, KIJANA BORA ANGEL GOMES!

Ander Herrera ametwaa Tuzo ya Sir Matt Busby inayoashiria yeye ndio Mchezaji Bora wa Mwaka wa Klabu ya Manchester United.

Herrera, ambae yuko kwenye Msimu wa 3 na Man United, aliwabwaga Antonio Valencia na Zlatan Ibrahimovic kwenye Kura zilizopigwa akizoa Kura 242 zaidi ya Valencia alieshika Namba 2.

Herrera, ambae amecheza Mechi 49 Msimu huu, ni Kiungo Mpiganaji aliekonga mioyo ya Mashabiki wengi kwa mtindo wake wa Uchezaji wa ‘Hapa Kazi Tu’!

Kiungo huyo, alieanza kuichezea Timu ya Taifa ya Kwanza ya Spain Novemba Mwaka Jana, anarithi Taji hili kutoka kwa Kipa David De Gea ambae ameshinda Tuzo hii mfululizo kwa Miaka Mitatu iliyopita.


JE WAJUA?
-Sir Matt Busby alikuwa ni Meneja wa zamani wa Manchester United alietumikia Vipindi Viwili vya 1945 hadi 1969 na kile cha 1970 hadi 1971.
-Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Man United ilibatizwa Jina la Sir Matt busby Mwaka 1996 kufuatia Kifo cha Meneja huyo Mwaka 1994.
-Tuzo yenyewe ni Mfano wa Sanamu ileile kubwa iliyosimikwa nje ya Uwanja wa Old Trafford upande wa Mashariki.



Akiongea mara baada ya kupokea Tuzo yake kwenye Sherehe iliyofanyika Old Trafford Jana Usiku, Herrera alinena: “Ni kitu spesho kushinda Tuzo hii hasa ukitazama Washindi wa Tuzo hii na hilo linakufanya ujue umuhimu wake. Na sasa nimesimamisha Rekodi ya David De Gea!”

Akaongeza: “Nahisi mapenzi ya Mashabiki na nawashukuru sana lakini nadhani Mchezaji wa Manchester United hasimami, lazima tuonyeshe upendo kwa Mashabiki kwani si Siku zote tunacheza vizuri lakini wanatupenda tu!”

De Gea, ambae ni Rafiki wa karibu wa Herrera ambae alikuwepo Stejeni, alieleza: “Yeye ni Mtu wa juu na ni Rafiki. Yeye ni Mchezaji anaecheza kwa Moyo wote Uwanjani na ni Mchezaji mzuri!”

Kwenye Tuzo nyingine, Henrikh Mkhitaryan alitunukiwa ile ya Goli Bora la Msimu kwa lile ‘Goli la N’nge’ alilofunga 26 Desemba 2016 Man United walipoipiga Sunderland 3-1.

Kijana Angel Gomes, anaechezea Kikosi cha U-18, kubeba ile ya Kijana Bora wa Mwaka.

MAN UNITED – TUZO MCHEZAJI BORA WA MWAKA -Washindi waliopita Miaka ya hivi karibuni:
MSIMU
MCHEZAJI
UTAIFA
2000–01
Teddy Sheringham
England
2001–02
Ruud van Nistelrooy
Netherlands
2002–03
Ruud van Nistelrooy
Netherlands
2003–04
Cristiano Ronaldo
Portugal
2004–05
Gabriel Heinze
Argentina
2005–06
Wayne Rooney
England
2006–07
Cristiano Ronaldo
Portugal
2007–08
Cristiano Ronaldo
Portugal
2008–09
Nemanja Vidić
Serbia
2009–10
Wayne Rooney
England
2010–11
Javier Hernández
Mexico
2011–12
Antonio Valencia
Ecuador
2012–13
Robin van Persie
Netherlands
2013–14
David de Gea
Spain
2014–15
David de Gea
Spain
2015–16
David de Gea
Spain
2016–17
Ander Herrera
Spain